Katika kile kinachoonekana kama kuwasha tochi kwenye giza ili kuona hazina iliyojificha, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed, ametoa rai nzito kwa wataalamu wa miamba nchini. Amesema wakati umefika kwa wajiolojia na watafiti wa ardhi kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wawe chachu ya mapinduzi ya kiuchumi ili kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Akiwa jijini Mbeya, "Jiji la Kijani" linalosifika kwa utajiri wa madini na vivutio vya kitalii, Mhandisi Zena alifungua Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania (TGS). Katika hotuba yake iliyojaa hamasa na maono, alisisitiza kuwa jiolojia ndio uti wa mgongo wa uchumi wa viwanda na ustawi wa jamii, akibainisha kuwa bila utafiti wa kina, rasilimali kama madini, gesi asilia, na maji zitabaki kuwa hadithi badala ya fedha mfukoni mwa Mtanzania.
Utafiti ni Dira, Sio Anasa
"Ndugu zangu wajiolojia, nyinyi ndio macho ya taifa ardhini. Tunategemea taarifa zenu sahihi ili tusiwe tunajenga nyumba juu ya migodi bila kujua. Fanyeni utafiti wa kutosha na mhakikishe matokeo hayo hayabaki kwenye makabrasha maabara, bali yawafikie wadau ili wafanye maamuzi sahihi ya kukuza uchumi," alisema Mhandisi Zena.
Kiongozi huyo aligusia changamoto kubwa inayojitokeza sasa ambapo wananchi, kwa kukosa taarifa, wanajikuta wakiweka makazi au miradi mingine juu ya maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini. Hali hii si tu inapoteza mapato ya taifa, bali pia inakwamisha mipango miji na uwekezaji wenye tija.
TGS: Jeshi la Wataalamu 4,000
Akielezea ukubwa wa jeshi hilo la wanasayansi, Rais wa TGS, Profesa Elisante Mshiu, alibainisha kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1968, chama hicho kimekua na sasa kina wanachama zaidi ya 4,000. Hawa ni 'vichwa' vilivyobobea kutoka vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi, ambao wamekuwa chachu ya uvumbuzi katika sekta ya nishati, maji, na madini.
"Dunia inakwenda kasi sana kiteknolojia. Kupitia jukwaa hili la TGS, tunabadilishana uzoefu na mbinu mpya za kisasa ili kuhakikisha Tanzania haiachwi nyuma katika uvunaji wa rasilimali zake," alisisitiza Prof. Mshiu.
Kilio cha Wachimbaji Wadogo Chunya na Mbeya
Akiwasilisha kilio cha 'mwananchi wa chini', Katibu Tawala Msaidizi (Uwekezaji, Viwanda na Biashara) wa Mkoa wa Mbeya, Bi. Anna Mwambene, aliwataka wataalamu hao kugeuza darubini zao kwa wachimbaji wadogo. Mkoa wa Mbeya na Songwe inajulikana kwa shughuli nyingi za uchorongaji, lakini wengi wanafanya kazi kwa kubahatisha.
"Wachimbaji wetu wadogo wanateseka. Mtu anachimba shimo kwa gharama kubwa, anakata tamaa na kuliacha, kumbe amebakisha hatua chache afikie mzigo (madini). Tunawaomba mshuke chini muwasaidie hawa ndugu zetu ili wachimbe kwa tija na kuacha kubahatisha," alisema Bi. Mwambene.
Kiwira na Ziwa Ngosi: Hazina ya Nishati
Kama sehemu ya mkutano huo, wajiolojia hao walitembelea vivutio vya kiuchumi na kitalii mkoani humo, ukiwemo Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira na Ziwa laajabu la Ngosi. Ziwa Ngosi, lililopo kileleni mwa mlima (Caldera), linatajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha nishati ya jotoardhi (Geothermal), nishati ambayo ni safi na endelevu kwa mustakabali wa taifa.
Tukio hili jijini Mbeya linatoa ishara kuwa Tanzania imedhamiria kutumia sayansi na teknolojia kama nyenzo kuu ya kufikia uchumi wa juu, huku wajiolojia wakiwa mstari wa mbele kuonyesha njia.