Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amezindua rasmi shughuli za uchimbaji madini katika mgodi wa Porcupine North, ulioko Makongorosi, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Mgodi huu unamilikiwa na Kampuni ya Shanta Gold Mining Limited. Waziri Mavunde alisema kuwa uzinduzi huo ni matokeo ya uamuzi wa Serikali, chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kurudisha leseni ya awamu ya sita ili kuhakikisha kuwa kuna utaratibu mzuri wa kuongeza mapato ya nchi kupitia sekta ya madini.
Waziri Mavunde aliyasema haya katika hafla ya uzinduzi wa shughuli za uchimbaji madini Porcupine North, iliyofanyika Kata ya Mkola, Makongorosi, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya.
"Eneo hili ni eneo ambalo leseni zake zilirudi serikalini kwa mujibu wa sheria. Baada ya kumalizika kwa kesi ya kimahakama na mwekezaji wa awali, Serikali iliweka utaratibu wa wazi wa kumpata mwekezaji atakayeendesha eneo hili la uchimbaji. Kampuni ya Shanta Gold Mining Limited ilishinda kwa masharti ya kuanza uchimbaji ndani ya miezi 18. Kwa sasa, mashapo yaliyothibitishwa yanafikia wakia 110,000, na kuna uwezekano baada ya utafiti zaidi kufikisha mashapo ya wakia 400,000. Kupitia mrabaha, kodi na tozo mbalimbali, hii itasaidia kuongeza makusanyo ya Serikali," alisema Mavunde.
Zaidi ya hayo, Waziri Mavunde aliongeza kuwa leseni moja iliyokuwa katika eneo la Saza, Mkoa wa Songwe, imekabidhiwa kwa wachimbaji wadogo. Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa kundi hili pia linanufaika na rasilimali za madini. Eneo hilo la Saza lililokabidhiwa kwa wachimbaji wadogo linakadiriwa kuwa na mashapo ya dhahabu yenye wakia laki mbili, ambayo thamani yake ni takriban shilingi trilioni 1.2 kwa bei ya sasa ya dhahabu.
"Mgodi huu pia utatoa fursa za ajira kwa Watanzania, utachangia maendeleo ya jamii kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), na utahakikisha kuwa kuna ushirikishwaji wa wazawa kupitia sera ya Local Content," aliongeza Mavunde.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, alisema kuwa uzinduzi wa shughuli za uchimbaji katika mgodi huo ni ushahidi wa mazingira mazuri ya uwekezaji nchini Tanzania chini ya uongozi na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake. Aliongeza kuwa mgodi huo utakuwa mfano wa kipekee nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Alhaji Mbaraka Alhaji Mbaraka Batenga, na kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda, waliwapongeza wananchi wa Kata ya Mkola kwa kuruhusu hatua hiyo kufikiwa na kwa kutoa ushirikiano kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo vya kata hiyo na taifa kwa ujumla.
"Tunakupongeza wewe binafsi Waziri Mavunde kwa kufuta leseni zilizokuwa hazifanyiwi kazi, ambazo baada ya kurudishwa Serikalini mnaendelea kuwapanga vyema wachimbaji wadogo," alisisitiza Alhaji Batenga.
Nao, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Shanta Gold Mining, Mhandisi Honest Mrema, na Meneja wa Mgodi wa New Luika Gold Mine unaomilikiwa na kampuni hiyo, Mhandisi Exeuper Lyimo, walitoa shukrani zao za dhati kwa Serikali kwa kupata leseni hizo na hatimaye kuanza uchimbaji na uzalishaji.
"Kupitia mgodi huu, kampuni imeongeza muda wa maisha ya migodi yake hapa nchini kutoka mwaka 2031 hadi 2034, na kupitia utafiti tunaondelea kufanya, muda wa maisha ya migodi utaongezeka zaidi. Lakini pia, shughuli za uchimbaji madini katika mgodi huu zitafanywa na kampuni za Kitanzania kwa asilimia 100. Mgodi wa New Luika umeajiri wafanyakazi 1140, ambapo asilimia 40 ni wakazi wanaozunguka eneo la mradi, na kuanza kwa mgodi huu kutasaidia kuongeza wafanyakazi zaidi ya 100, ambapo asilimia 60 yao ni vijana kutoka katika maeneo haya ya Porcupine," aliongeza Mhandisi Mrema.