Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameibua kashfa nzito ndani ya Mahakama Kuu ya Tanzania baada ya kuhoji uhalali wa kesi ya uhaini inayomkabili, akifichua kuwepo kwa ratiba inayoonyesha tarehe ya kutolewa hukumu kabla hata ya shahidi mmoja kusikilizwa.
Katika kile kilichoonekana kama kuweka mahakama yenyewe kizimbani, Lissu aliwasilisha hoja tatu nzito mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akitaka ufafanuzi kabla ya kesi kuendelea. Hoja yake ya kutisha zaidi ilikuwa ni kuhusu ratiba aliyopewa kutoka kwa Naibu Msajili, ambayo ilipanga usikilizwaji wa mashahidi hadi Novemba 11, 2025, na kisha kuweka Novemba 12, 2025 kama tarehe ya hukumu.
"Mheshimiwa Jaji, leo ni Oktoba 6, hatujasikiliza hata shahidi mmoja. Hii hukumu ya Novemba 12 inatoka wapi?" alihoji Lissu kwa ukali. "Kama hukumu tayari ipo, basi itolewe sasa hivi nijue moja. Kama ni kunyongwa, ninyongwe, au la, tujue," aliongeza, kauli iliyoacha ukumbi mzima kimya.
Hoja ya pili ya Lissu ilikuwa ni kuhusu ulinzi mkali na kuzuiliwa kwa watu aliowaorodhesha kuhudhuria kesi yake, licha ya kuagizwa na mahakama awasilishe majina 100. Alieleza kwa uchungu jinsi ndugu yake aliyesafiri kutoka Ujerumani alivyozuiwa getini, pamoja na wengine kupigwa. "Nataka kujua, hii ni Mahakama ya Polisi au Mahakama ya Tanzania? Nani ana mamlaka ya kuamua nani aingie hapa ndani? Ni nyie majaji au wale wanaonishtaki?" aliuliza.
Aidha, alitaka ufafanuzi kuhusu barua iliyomtaka ashiriki "kikao cha maandalizi" (pre-session meeting) kwa njia ya mtandao akiwa gerezani, utaratibu ambao alisema hauufahamu.
Kutokana na uzito wa hoja hizo, jopo la majaji lililazimika kuahirisha shauri hilo kwa nusu saa ili kujadiliana na kutoa ufafanuzi, huku Lissu akiwa amefanikiwa kugeuza kesi dhidi yake na kuwa kesi ya kuhoji uhuru na haki ndani ya mfumo wa sheria nchini.