Lissu Atinga Mahakamani, Acharuka: 'Kesi Irushwe Live, Mimi Siyo Mwenzao, Niiteni Mshtakiwa'

politics | Thu Sep 18 2025


Lissu Atinga Mahakamani, Acharuka: 'Kesi Irushwe Live, Mimi Siyo Mwenzao, Niiteni Mshtakiwa'

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameibua hoja nzito mbele ya jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi ya uhaini inayomkabili, akidai mambo mawili makuu: kesi yake irushwe mubashara na upande wa mashtaka uache kumwita "mwenzetu". Lissu alitoa madai hayo jana katika Mahakama Kuu, kabla hata ya hoja za kisheria kuhusu kesi yenyewe kuanza kujadiliwa.


Akisimama mbele ya Majaji Dunstan Ndunguru, James Karayemaha, na Ferdinand Kiwonde, Lissu alisema amewasilisha ombi rasmi kwa Msajili wa Mahakama tangu Septemba 4, 2025, la kutaka kesi yake itangazwe moja kwa moja kwenye vyombo vya habari, lakini hadi sasa hajapata majibu. Alisema lengo la ombi hilo ni kuwaepusha wafuasi wake na kile alichodai ni vipigo kutoka kwa polisi wanapofika mahakamani kufuatilia kesi.


"Waheshimiwa majaji, nikiwa gerezani napata taarifa za watu wangu wanavyopigwa huko nje. Ili kumaliza tatizo hili, ruhusuni kesi hii ionyeshwe mubashara ili watu waifuatilie popote walipo bila kufika hapa na kupigwa. Hili jambo halileti picha nzuri kwa nchi yetu," alisisitiza Lissu.


Hoja ya pili iliyozua mvutano mdogo mahakamani ni pale Lissu alipomvaa Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, akimtaka aache kumrejelea kama "mwenzetu". Lissu alidai kuwa yeye yuko mahakamani kama mtuhumiwa wa kosa la jinai la uhaini, hivyo si mwenzao na anapaswa kuitwa kwa hadhi yake ya "mshtakiwa".


"Wakili Katuga ananiita 'mwenzetu' mara kwa mara. Namwambia wazi, mimi siyo mwenzao. Mimi ni mshtakiwa na nataka niitwe hivyo," alisema Lissu kwa ukali.


Jaji Ndunguru aliingilia kati na kumwelekeza Wakili Katuga kuheshimu ombi la mshtakiwa. Akijitetea, Wakili Katuga alisema alitumia neno hilo kwa heshima ya kitaaluma, kwani Lissu mwenyewe alijitambulisha kama wakili wa miaka 20, lakini akakubali kufuata maelekezo ya mahakama.


Kuhusu ombi la kesi kurushwa mubashara, Jaji Ndunguru alisema suala hilo lipo ndani ya mamlaka ya mahakama na watalitolea maelekezo rasmi baadaye.


Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini, akidaiwa kutoa maneno ya uchochezi Aprili 3, 2025, yaliyolenga kuhamasisha umma kuzuia na kuvuruga Uchaguzi Mkuu.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.