Hali ya mivutano na mabishano ya kisheria ilitawala katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kugoma kuendelea na usikilizwaji wa kesi ya uhaini inayomkabili. Lissu alichukua hatua hiyo akipinga kile alichodai kuwa ni amri ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZDCO) ya kuwaondoa mahakamani wafuasi wa chama chake waliokuja kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.
Awali, shamrashamra zilianza pale baadhi ya viongozi wa chama, akiwemo Godbless Lema, walipowahimiza wanachama waliokuwa ndani ya chumba cha mahakama watoke nje kama ishara ya kupinga wenzao kuzuiwa kuingia. Kitendo hiki kilileta usumbufu na kusababisha shughuli za kimahakama kusimama kwa muda.
Akiwasilisha hoja zake mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, Lissu alisisitiza kuwa kesi inayomkabili ni ya umma na yenye maslahi ya kitaifa, hivyo haiwezi kuendeshwa kwa siri huku wananchi wakinyimwa haki yao ya msingi ya kushuhudia. Aliitaka mahakama kuahirisha kesi na kutoa amri ya kuwaruhusu wafuasi wake warejee ndani, akisema kuendelea bila wao ni sawa na kuendesha kesi gizani.
Hata hivyo, upande wa mashtaka, ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Nassoro Katuga, ulipinga vikali hoja hizo. Katuga alidai kuwa hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa kuthibitisha kuwepo kwa amri ya polisi ya kumtoa mtu yeyote nje ya mahakama. Alisema kesi haiwezi kusimama kwa sababu tu ya kutokuwepo kwa hadhira, kwani sheria haielekezi hivyo.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili, jopo la majaji lilitupilia mbali ombi la Tundu Lissu. Katika uamuzi wake, Jaji Ndunguru alibainisha kuwa mahakama haikupokea ushahidi wowote wa kuthibitisha madai ya kuwepo kwa amri ya polisi. Badala yake, ilionekana kuwa watu waliondoka kwa hiari yao kufuatia hamasa kutoka kwa viongozi wao. Kufuatia uamuzi huo, hali ilitulia na wafuasi waliokuwa nje walirejea ndani, na kesi iliendelea huku Lissu akiendelea kuwasilisha pingamizi zake dhidi ya hati ya mashtaka.