Serikali ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) imetoa tamko kali la kulaani mwendelezo wa kile ilichokitaja kama "mauaji ya kinyama" yanayotekelezwa kupitia matumizi ya silaha nzito za kisasa, zikiwemo ndege zisizo na rubani (drones), dhidi ya raia wasio na hatia katika maeneo yenye mzozo ya Mashariki mwa nchi hiyo.
Katika taarifa iliyojaa masikitiko na onyo kali, Serikali ya Kinshasa imebainisha kuwa mashambulizi hayo ya anga yamegeuka kuwa janga la kibinadamu, yakisababisha vifo vya takriban watu 100 katika muda mfupi uliopita. Hali ni mbaya zaidi kwa maelfu ya wananchi waliojeruhiwa, huku idadi ya waliolazimika kuyakimbia makazi yao na kugeuka wakimbizi wa ndani ikitajwa kupindukia 200,000.
Msemaji wa Serikali ya DRC, Bwana Patrick Muyaya, amekemea vikali vitendo hivyo akisema vinalenga kuvuruga amani katika mikoa ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikigubikwa na moshi wa vita. Muyaya amesisitiza kuwa matumizi haya ya nguvu ni ukiukwaji wa wazi na wa makusudi wa makubaliano ya kusitisha mapigano, hususan yale ya 'Makubaliano ya Washington' yaliyosimamiwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.
"Huku ni kuchezea amani na dharau kwa jumuiya ya kimataifa. Mashambulizi haya yanayolenga raia na hata kutishia usalama wa nchi jirani ya Burundi ni mpango mahususi wa kuisambaratisha Kanda ya Maziwa Makuu na kuleta mkanganyiko usioisha," alikaririwa Muyaya akionya juu ya hatari ya mzozo huo kusambaa kikanda.
Kinshasa imeitaka jumuiya ya kimataifa kutofumba macho dhidi ya ukatili huu na badala yake iweke vikwazo vizito kwa wahusika wote wanaoharibu juhudi za kidiplomasia zilizosifiwa duniani kote. Serikali imewataka wananchi wa DRC kuweka tofauti zao pembeni na kuungana kwa moyo wa kizalendo ili kukabiliana na kile inachokiita "uvamizi wa Rwanda", ikidai kuwa nchi hiyo jirani ndiyo inayochochea machafuko hayo.
Hata hivyo, kwa upande wa pili wa sarafu, Serikali ya Rwanda kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje imeruka kimanga tuhuma hizo. Kigali imekanusha vikali kuhusika kwa namna yoyote na mashambulizi hayo ya 'drones' au uvunjaji wa makubaliano ya amani, ikisisitiza kuwa shutuma za DRC ni propaganda zisizo na mashiko wala ushahidi wa kutosha.
Mvutano huu mpya kati ya Kinshasa na Kigali unazidi kuweka rehani usalama wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Kadri siku zinavyosonga, ndivyo hali ya sintofahamu inavyozidi kutanda, huku sauti za vilio vya wanawake na watoto zikiendelea kusikika katika milima na mabonde ya Mashariki mwa Kongo, wakisubiri nusura ya jumuiya ya kimataifa kumaliza vita hii ya maneno na silaha.