Mithali ya wahenga isemayo "haraka ya kupa haina baraka" imeonekana kutimia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), baada ya matumaini ya amani kugeuka kuwa simanzi nzito. Saa chache tu baada ya wino kukauka kwenye mkataba wa amani uliopigiwa debe na Rais wa Marekani, Donald Trump, mapigano makali yamezuka upya na kusababisha umwagikaji wa damu wa kutisha katika Jimbo la Kivu Kusini, jambo linaloashiria kuwa safari ya amani kwa jirani zetu bado ni ndefu na yenye miiba.
Taarifa za kusikitisha zilizotolewa jana na Msemaji wa Serikali katika Jimbo la Kivu Kusini, zimeeleza kuwa zaidi ya raia 413 wamepoteza maisha katika miji ya Bukavu na Uvira. Maeneo haya, ambayo ni vitovu muhimu vya biashara vinavyopakana na nchi za Maziwa Makuu, yamegeuka kuwa machinjio badala ya makazi.
"Inasikitisha kueleza kuwa idadi ya vifo imepindukia watu 413. Kinachoumiza zaidi ni kwamba waliouawa si wanajeshi, bali ni makundi yasiyo na hatia wakiwemo wanawake, watoto wadogo na vijana. Wameuawa kikatili kwa risasi za moto, mabomu ya kutupa kwa mkono na milipuko mingine," alieleza msemaji huyo kwa uchungu.
Serikali ya Kinshasa imenyoshea kidole chake cha lawama moja kwa moja kwa nchi jirani ya Rwanda. Wanadai kuwa vikosi vilivyoshambulia miji hiyo si waasi wa M23 pekee, bali vimejumuisha vikosi maalum vya Jeshi la Rwanda (Special Forces) na mamluki wa kigeni. "Hawa wavamizi wamepuuza makubaliano yote ya amani na wanaendesha operesheni za kuangamiza watu wetu bila huruma," ilisema taarifa hiyo ya serikali.
Kinachofanya tukio hili kuwa la kushangaza na la kusikitisha zaidi ni muda uliotokea (timing). Mashambulizi haya ya M23 yalianza tarehe 5 Desemba, ikiwa ni siku moja tu baada ya sherehe kubwa ya utiaji saini wa mkataba wa amani kati ya DRC na Rwanda, chini ya upatanishi mzito wa Rais Donald Trump. Mkataba huo ulibeba ahadi nono za usitishaji vita wa kudumu, upokonyaji silaha kwa makundi ya waasi, na mpango wa kuwarejesha wakimbizi makwao. Lakini sasa, makubaliano hayo yanaonekana kuwa "amani ya karatasi" huku uhalisia ardhini ukiandikwa kwa damu.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN) wameonya kuwa hali ni mbaya, huku wakikadiria kuwa kundi la M23 linapata nguvu kutoka kwa takriban wanajeshi 4,000 wanaodaiwa kutoka Rwanda. Pande zote mbili, Kinshasa na Kigali, zinaendelea kutupiana mpira wa lawama, kila upande ukimshutumu mwenzake kwa kukiuka mkataba huo mpya.
Jumuiya ya Kimataifa imeingiwa na taharuki. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametoa wito wa dharura wa kutaka uhasama huo ukomeshwe mara moja bila masharti. Naye Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Mahmoud Ali Youssouf, amelaani vikali mauaji ya raia na kutaka suluhu ya kisiasaipewe kipaumbele badala ya mtutu wa bunduki.
Hofu imeanza kutanda kuwa vita hivi vinaweza kusambaa na kuifanya kanda nzima ya Afrika Mashariki na Kati kuwa isiyotawalika. Nchi ya Burundi sasa imeingia kwenye rada ya hatari. Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Edouard Bizimana, ameonya kuwa kuanguka kwa mji wa Uvira mikononi mwa waasi ni tishio la moja kwa moja kwa mji mkuu wa kiuchumi wa Burundi, Bujumbura. Ikumbukwe kuwa Burundi ina mkataba wa kijeshi na DRC na tayari ina askari wapatao 18,000 mpakani, jambo linaloashiria uwezekano wa vita kupanuka.
Eneo la Mashariki mwa Kongo, lenye utajiri mkubwa wa madini ambayo yanatajwa kama "laana ya utajiri," limekuwa uwanja wa vita kwa zaidi ya makundi 100 ya wanamgambo. Shirika la UNHCR linakadiria kuwa mzozo huu wa muda mrefu tayari umesababisha zaidi ya watu milioni 7 kukimbia makazi yao, idadi ambayo inazidi kuongezeka kila uchao huku matumaini ya amani yakizidi kufifia.