Figisufigisu za Kura za Maoni Zafufua Hoja ya Mgombea Huru

politics | Wed Aug 27 2025


Figisufigisu za Kura za Maoni Zafufua Hoja ya Mgombea Huru

Wakati vyama vya siasa nchini vikikamilisha michakato yake ya ndani ya kuteua wagombea watakaozipigania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao, kumesalia na kovu la sintofahamu na manung'uniko miongoni mwa wanachama. Madai ya upendeleo na kuenguliwa kwa wagombea walioshinda kura za maoni kumesababisha baadhi ya wanachama kukihama vyama vyao huku wengine wakibaki na vinyongo, hali iliyofufua upya mjadala mzito kuhusu umuhimu wa kuruhusu mgombea huru katika siasa za Tanzania.


Wachambuzi wa siasa na wadau mbalimbali wanaona kuwa kuruhusu wagombea binafsi kugombea nafasi za uongozi ndio "mwarobaini" wa tatizo hili la kila baada ya miaka mitano. Wanasema mfumo huu utatoa fursa kwa wagombea wanaokubalika na wananchi lakini hawapendwi na viongozi wa vyama vyao kuweza kupata haki yao ya kikatiba ya kuchaguliwa.


Mbunge wa zamani wa Moshi Mjini kupitia TLP, Thomas Ngawaiya, ni mmoja wa wanaoamini kuwa Tanzania imechelewa mno katika hili. Anakumbushia kisa kilichomkuta mwaka 2005 ambapo alishika nafasi ya kwanza kwenye kura za maoni lakini chama kikamteua aliyeshika nafasi ya tatu, na matokeo yake jimbo hilo likachukuliwa na upinzani. "Mwarobaini wa tatizo hili ni mgombea huru. Kama chama kinakuacha na wananchi wanakupenda, unapata fursa ya kugombea," anasema Ngawaiya, ambaye sasa ni kada wa CCM.


Hata hivyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Annanilea Nkya, anasema suluhisho si tu mgombea huru, bali ni mabadiliko makubwa na ya kweli ya kidemokrasia. Anahoji kuwa hata baada ya miaka 30 ya mfumo wa vyama vingi, siasa za nchi bado zinaendeshwa kimfumo wa chama kimoja. "Mgombea huru ni hitaji la muda mrefu, lakini pia tunahitaji demokrasia ya kweli. Watu wanaoteuliwa sasa wengine wanahusishwa na rushwa, hivyo asiye na fedha za kuhonga hawezi kupata uongozi," anafafanua Annanilea.


Mtazamo huu unapewa uzito wa kihistoria na mchambuzi wa siasa, Gwandumi Mwakatobe, anayeeleza kuwa hoja ya mgombea huru si ngeni. Anasema ilikuwepo tangu mwaka 1995 na iliungwa mkono na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Aidha, suala hili lilikuwa sehemu ya mapendekezo muhimu katika Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba.


Mwakatobe anafananisha uanachama wa vyama vya siasa na "kifungo," ambapo wanasiasa wengi wamebanwa na hawawezi kutoka hata wanapoenguliwa isivyo haki. "Kimsingi, vyama vinaogopa kupoteza watu, ndio maana kuna kigugumizi. Kuruhusu mgombea huru kutawafungua wanasiasa wengi na kuwapa wananchi fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka, hata kama hawapendi kuwa wanachama wa chama chochote," anamalizia Mwakatobe.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.