Waziri Mkuu mstaafu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, ametoa tathmini yake kuhusu kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka huu, akisema vyama vya upinzani havina nafasi ya kushinda kiti cha urais kutokana na kile alichokiita kutojipanga kikamilifu. Badala yake, amevishauri vielekeze nguvu zao katika kupambania nafasi za ubunge na udiwani ili kujijenga kisiasa.
Katika mahojiano maalum, Sumaye alifunguka kuwa anaona Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiwa kimejipanga vyema na kinaendelea na kampeni zake kwa nguvu, tofauti na vyama vya upinzani ambavyo havionyeshi msisimko wa kutosha. "Unaona CCM wako kazini muda wote, wana mikutano yao na wanachama zaidi ya milioni 13. Upinzani unaonekana kujitokeza wakati wa uchaguzi tu, hali inayopunguza sana dalili za ushindi. Wanapaswa kufanya kazi ya kisiasa ya kujitambulisha kwa wananchi kabla ya uchaguzi," alisema Sumaye.
Aidha, alimzungumzia mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, akisema ni mgombea imara anayeuzika kwa urahisi kutokana na kuwa na mambo mengi ya kuwaeleza wananchi ambayo ameyafanya na anayopanga kuyafanya, jambo linalompa nguvu kubwa kwenye kampeni.
Katika hatua nyingine, Sumaye alionesha masikitiko yake juu ya jinsi siasa za sasa zilivyogeuka kuwa biashara ya wenye fedha. Alikumbushia enzi zake alipogombea ubunge mwaka 1985 akiwa na Shilingi 10,000 tu mfukoni, kiasi alichokipata baada ya kukopa mshahara wa miezi miwili. "Siasa za sasa zimekuwa biashara. Mtu anaambiwa kama hana milioni 300 au 500 asijaribu kugombea. Wakati wangu, niliingia bungeni na shilingi elfu kumi tu. Chama na wananchi ndio walikuwa wanagharamia kila kitu, hata chakula mgombea alikuwa analishwa na wananchi, hakukuwa na mianya ya rushwa," alikumbushia Sumaye.
Alifafanua kuwa zamani, chama kilisimamia wagombea wote kwa usawa, wakiwekwa kwenye nyumba moja ya wageni na kula pamoja, jambo lililozuia kabisa fursa za kutoa rushwa kwa wapiga kura.
Licha ya tathmini yake ya kisiasa, Sumaye alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa Watanzania wote kudumisha amani na utulivu wakati na baada ya uchaguzi. Alisisitiza kuwa Tanzania inajulikana kama kisiwa cha amani na mshikamano, hivyo hakuna sababu ya kuruhusu tofauti za kisiasa zivuruge tunu hiyo ya taifa. "Uchaguzi utapita na siasa zitaendelea kuwepo. Hata kama hujaridhidika na matokeo, bado kuna fursa ya kujipanga kwa wakati mwingine. Tusifanye fujo wala jambo lolote litakalohatarisha amani yetu," alisisitiza.