Katika kile kinachoonekana kama "Kufumua na kushona upya" mkakati wa biashara, kampuni ya Meta (wamiliki wa Facebook, Instagram, na WhatsApp) imeamua kuingia vitani mzimamzima. Taarifa za ndani kutoka Silicon Valley zinaeleza kuwa maabara maalum ya kampuni hiyo, Meta Superintelligence Lab (MSL), iko jikoni ikiandaa mapishi mapya mawili yenye majina ya kudadisi: ‘Mango’ (Embe) na ‘Avocado’ (Parachichi).
Hii si habari ya kupuuzia kwa wadau wa teknolojia nchini Tanzania, hasa wale wanaotegemea mitandao ya kijamii kuendesha biashara zao, kwani maboresho haya yanatarajiwa kubadili namna tunavyotumia mitandao hiyo pendwa.
Siri ya 'Embe' na 'Parachichi' Yafichuka
Kwa mujibu wa duru za kuaminika zilizonukuliwa na Wall Street Journal, wakuu wa Meta, Alexandr Wang (Afisa Mkuu wa AI) na Chris Cox (Afisa Mkuu wa Bidhaa), wameanika ramani ya vita hii mpya. Mkakati wao umelenga eneo moja kuu: Kuunda mifumo ya Akili Mnemba (AI) yenye uwezo wa kutengeneza picha na video za hali ya juu, pamoja na mifumo ya lugha (LLM) inayoweza kushindana na ile ya washindani wao.
- Mango (Embe): Hii ni kete mpya ya Meta kwenye ulimwengu wa video na picha. Lengo ni kuleta ushindani dhidi ya programu ya 'Sora' ya OpenAI na 'Veo 3' ya Google. Mfumo huu unatarajiwa kuwezesha watumiaji wa Instagram na Facebook kutengeneza video za maajabu kwa kutumia maelezo ya maandishi tu. Hii ni hatua muhimu kuelekea kile kinachoitwa "World Model"—mfumo wa kidijitali unaoiga uhalisia wa dunia tunayoishi.
- Avocado (Parachichi): Hili ni jina la siri la toleo jipya la mfumo wa lugha (LLM). Tofauti na matoleo ya nyuma ya Llama, 'Avocado' inatajwa kuwa na makali zaidi kwenye eneo la uandishi wa kodi za kompyuta (coding), eneo ambalo Meta ilikuwa imepigwa bao na washindani wake.
Maboresho haya yatatufikia lini?
Wataalamu hao wamebainisha kuwa matunda haya ya kidijitali yataiva na kuwa tayari kuliwa (kuzinduliwa) katika nusu ya kwanza ya mwaka ujao (2026). Hii inamaanisha kuwa kuanzia mwakani, status zako za WhatsApp na reels za Instagram zinaweza kuwa na muonekano wa kipekee kabisa unaotengenezwa na AI.
Siasa za Ndani na Ondoko la Yann LeCun
Jambo la kushangaza ni uwezekano wa Meta kubadili msimamo wake wa siku zote wa "Open Source" (Programu Huria). Imeelezwa kuwa endapo 'Avocado' itaonyesha uwezo mkubwa wa kipekee uliopitiliza, Meta inaweza kuifanya kuwa ya kulipia au ya siri (closed source), kinyume na desturi yao ya kugawa teknolojia bure.
Hali hii inakuja wakati ambapo nguli wa AI, Yann LeCun, anatajwa kuwa mbioni kuondoka kufuatia mabadiliko haya ya kimkakati. Inaonekana kuingia kwa damu mpya kama Alexandr Wang, aliyesajiliwa kwa dau kubwa na Mark Zuckerberg, kumeleta msuguano na watafiti wa zamani, lakini pia kumeleta kasi mpya. Ushahidi wa kasi hiyo ni programu ya video ya 'Vibe' iliyozinduliwa na MSL mwezi Septemba, ambayo tayari imekonga nyoyo za watumiaji zaidi ya milioni 2 kila siku.
Mwaka 2026: Mwaka wa Kibabe
Mwaka ujao unatazamiwa kuwa uwanja wa "Fahali Wawili". Wakati Meta ikinoa 'Mango' na 'Avocado', washindani wao hawajalala. OpenAI inatarajiwa kuachia "mzigo" mpya mwezi Januari, huku tajiri Elon Musk naye akitamba kuleta 'Grok 5' kabla ya mwezi wa sita.
Kwa sisi watumiaji wa hapa nyumbani, vita hii ya tembo itatunufaisha sisi nyasi. Tutarajie simu zetu kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kufanya kazi, kubuni, na kutuhudumia. Je, uko tayari kwa mapinduzi ya 'Embe' na 'Parachichi'?