Dunia ya teknolojia imepigwa na butwaa nyingine, safari hii ikimhusisha mmoja wa "Miungu Watu" wa Akili Mnemba (AI). Yann LeCun, Mwanasayansi Mkuu wa Meta (kampuni mama ya Facebook, Instagram, na WhatsApp) na mshindi wa tuzo ya heshima ya Turing, ametangaza rasmi mpango wake wa kuondoka kwenye himaya ya Mark Zuckerberg ili kuanzisha mapinduzi mapya. Hatua hii inaashiria mabadiliko makubwa katika uelekeo wa teknolojia duniani, huku akili ikihamia kwenye mifumo inayoelewa dunia badala ya kukariri maneno.
Dau la Kufuru: Trilioni 9 Mezani
Taarifa za uhakika kutoka jarida la Financial Times zinaeleza kuwa LeCun yuko katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kusaka mtaji wa awali (seed funding) wa kiasi cha Euro Milioni 500. Kwa fedha za madafu, hii ni takriban Shilingi za Kitanzania Trilioni 1.5.
Lengo la mkwanja huu mrefu ni kuipa thamani kampuni yake mpya, AMI Labs (Advanced Machine Intelligence Labs), kufikia thamani ya Euro Bilioni 3 (sawa na takriban Shilingi za Kitanzania Trilioni 9). Hiki ni kiasi ambacho kinaweza kuendesha bajeti za wizara kadhaa hapa nchini kwa mwaka mzima, likiwa ni dau la kihistoria kwa kampuni inayoanza (startup).
Kwaheri Silicon Valley, Karibu Paris
LeCun, ambaye ni raia wa Ufaransa, ameamua kuipa mgongo Silicon Valley ya Marekani na kuweka makao makuu ya AMI Labs jijini Paris. Sababu yake ni nzito na yenye kufikirisha: Anaamini kuwa Silicon Valley "imelewa sifa" na kuzama kwenye wimbi la mifumo ya kuzalisha maandishi (Generative AI) kama ChatGPT, huku wakisahau picha kubwa ya sayansi.
"Silicon Valley wamezama kabisa kwenye generative models," alikaririwa akisema. LeCun anaamini mustakabali wa AI siyo 'chatbots' zinazopiga gumzo, bali ni "World Models"—mifumo inayoelewa jinsi dunia inavyofanya kazi kifizikia, kimantiki na kiuhalisia, kama vile binadamu au mnyama anavyojifunza.
Timu ya Ushindi: Lebrun Apewa Usukani
Ili kuhakikisha jahazi hili jipya halizami, LeCun amemnasa Alexandre Lebrun, mwanzilishi wa kampuni ya afya ya Nabla, kuwa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa AMI Labs. LeCun mwenyewe atashika nafasi ya Uwenyekiti huku akiendelea kutoa dira ya kiufundi. Muungano huu wa kimkakati kati ya AMI Labs na Nabla unatazamiwa kuleta mapinduzi makubwa, hasa ikizingatiwa uzoefu wa Lebrun katika kuendesha makampuni ya teknolojia.
LeCun anatarajiwa kuondoka Meta mwishoni mwa mwaka huu na kuanza rasmi kazi AMI Labs mwezi Januari 2026. Hii inahitimisha kipindi chake cha miaka 12 ndani ya Meta, ambapo alikuwa nguzo kuu ya maendeleo ya AI.
Wimbi la Wataalamu Kujitenga
Hatua ya LeCun inafuata nyayo za vigogo wengine walioamua kujiondoa kwenye makampuni makubwa ili kuanzisha 'Vyuma' vyao.
- Ilya Sutskever: Aliyekuwa Mwanasayansi Mkuu wa OpenAI, alianzisha Safe Superintelligence (SSI) na kupata mtaji wa Dola Bilioni 1 (takriban TZS Trilioni 2.7) kwa thamani ya kampuni ya Dola Bilioni 5.
- Mira Murati: Aliyekuwa CTO wa OpenAI, ameanzisha Thinking Machine Labs na kusaka mtaji wa Dola Milioni 100 kwa thamani kubwa.
- Fei-Fei Li: 'Mama wa AI' kutoka Chuo cha Stanford, naye alianzisha World Labs inayoshindana moja kwa moja na wazo la LeCun, ikiwa na thamani ya Dola Bilioni 1.
Tufarajike na Nini Watanzania?
Hii inatufundisha kuwa teknolojia haisimami. Wakati sisi tunashangaa ChatGPT, wenzetu wameshavuka huko na sasa wanatengeneza "World Models" (Mifumo ya Ulimwengu). Tofauti na AI ya sasa inayotabiri neno lifuatalo, World Models zitakuwa na uwezo wa kupanga, kufikiri, na kuelewa matokeo ya vitendo katika ulimwengu halisi.
Kwa wabunifu na vijana wa Kitanzania, huu ni wakati wa kufungua macho. Fursa za uwekezaji katika AI zinazidi kukua, na Paris inageuka kuwa kitovu kipya cha teknolojia Ulaya. "Mchumia juani, hulia kivulini"—LeCun ameamua kutoka juani kwa Zuckerberg na kwenda kutengeneza kivuli chake mwenyewe.