Google na Samsung Waunganisha Nguvu: Miwani ya 'Gemini' Kutua 2026, Zuckerberg Apewa Changamoto Mpya

it | Wed Dec 10 2025


Google na Samsung Waunganisha Nguvu: Miwani ya 'Gemini' Kutua 2026, Zuckerberg Apewa Changamoto Mpya

Vita ya kuteka soko la vifaa vinavyovaliwa (Wearables) imezidi kupamba moto. Kampuni ya Google imetangaza rasmi kuwa itaingiza sokoni miwani yake mipya janja (Smart Glasses) inayotumia akili ya Gemini AI ifikapo mwaka 2026.


Katika hatua inayoashiria ushindani mkali dhidi ya Meta (wamiliki wa Facebook/Instagram) na miwani yao ya Ray-Ban, Google imeungana na wababe wa Korea Kusini, Samsung Electronics, pamoja na kampuni za Warby Parker na Gentle Monster kutengeneza kifaa hiki cha kisasa.


Gemini Ndani ya Macho Yako


Tangazo hili lililotolewa Jumatatu (Desemba 8) linaweka wazi kuwa miwani hii itakuja katika aina mbili:


  1. Miwani ya Sauti (Audio-only): Hii haina kioo (display). Inakuruhusu kuongea na Gemini, kusikiliza muziki, na kupokea majibu ya sauti. Hii ndiyo itatangulia kutoka mwakani.
  2. Miwani ya Kioo (Display AI Glasses): Hii ina kioo kidogo ndani ya lenzi kinachokuonyesha taarifa kama ramani (AR Maps), ujumbe, au tafsiri ya lugha unapoongea na mtu wa lugha nyingine.


Google vs Meta: Mbinu Tofauti


Tofauti na miwani ya Meta ambayo inajaribu kuweka "kompyuta nzima" kwenye miwani (standalone), Google wameamua kutumia njia tofauti. Miwani yao itategemea nguvu ya simu yako ya mkononi (imeunganishwa bila waya).


Google inasema wamefanya hivi ili:


  1. Kuhakikisha miwani inakuwa nyepesi na inakaa usoni kama miwani ya kawaida.
  2. Kuifanya betriidumu muda mrefu kwa kuiachia simu ifanye kazi nzito ya kuchakata data.


'Project Aura' na Xreal: Uhalisia Ulioboreshwa


Mbali na miwani ya Samsung, Google pia imeshirikiana na kampuni ya China ya Xreal katika mradi uitwao 'Project Aura'. Hii ni miwani mikubwa kidogo inayolenga kuonyesha picha za kidijitali juu ya ulimwengu halisi (See-through AR).


Sifa zake ni:


  1. Inaunganishwa na waya (kebo) kwenye betri ya nje.
  2. Ina wigo mpana wa kuona (70-degree field of view).
  3. Inaweza kutambua ishara za mikono (Hand tracking), sawa na teknolojia ya Apple Vision Pro.


Samsung Galaxy XR Yapewa Maboresho


Wakati tunasubiri miwani hiyo ya 2026, Google imetangaza maboresho makubwa kwa kifaa cha Galaxy XR (kilichotoka Oktoba na Samsung):


  1. Travel Mode (Hali ya Kusafiri): Sasa unaweza kutumia kifaa hiki kwenye gari au ndege bila picha kuyumba yumba.
  2. PC Connect: Unaweza kuunganisha kifaa hiki na kompyuta yoyote ya Windows na kuona skrini ya kompyuta yako kwenye miwani kwa ukubwa wa sinema. Hii inafaa kwa kazi na michezo (Games).
  3. Likeness (Avatar Halisi): Ukijipiga picha usoni na simu, teknolojia hii inatengeneza katuni (Avatar) inayofanana na wewe na kuiga matendo yako wakati wa mikutano ya video (Virtual Meetings).


2026: Mwaka wa Vita ya Miwani


Soko la miwani janja linatarajiwa kulipuka mwaka 2026.


  1. Meta: Wanaendelea kuboresha miwani yao na wako mbele kwa sasa.
  2. Google/Samsung: Wanakuja na nguvu ya Gemini.
  3. Apple: Inasemekana watatoa miwani yao ya kwanza mwishoni mwa 2026.
  4. Alibaba: Kampuni hii ya China nayo inapanua mbawa zake kimataifa.


Kwa mtumiaji wa Kitanzania, hii inamaanisha huko tuendako, huenda simu za mkononi zikaanza kupungua umaarufu, na badala yake tutakuwa tunatembea na "Akili Mnemba" machoni mwetu, tukipata ramani za Google Maps au kutafsiri lugha bila kugusa mfukoni.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.