Hali ya hewa si shwari ndani ya himaya ya Meta, kampuni mama inayomiliki mitandao pendwa hapa Tanzania ya Facebook, Instagram, na WhatsApp. Wakati Mark Zuckerberg akiendelea kusukuma ajenda yake ya kuwekeza matrilioni kwenye Akili Mnemba (AI), shinikizo kubwa kutoka kwa wawekezaji na wanahisa limeanza kusababisha "kufumuka kwa nyuzi" katika safu ya juu ya uongozi wa kampuni hiyo.
Ripoti za hivi punde zinaonyesha wimbi la kuondoka kwa vigogo (High-profile departures) ambao wameitumikia kampuni hiyo kwa miaka mingi, hali inayoashiria kuwa mabadiliko makubwa na yenye maumivu yanafanyika ili kukidhi kiu ya gharama kubwa ya teknolojia mpya.
Vigogo Wanaaga: Mwisho wa Enzi
Taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo vya kuaminika kama Bloomberg zimethibitisha kuwa John Hegeman, Afisa Mkuu wa Mapato (CRO) wa Meta, ametangaza kuondoka. Hegeman si mtu mdogo; amekuwa na Meta kwa miaka 17, akishuhudia ukuaji wa kampuni hiyo tangu enzi za Facebook ikiwa mtandao wa vijana wa vyuo hadi kuwa himaya ya dunia. Anaondoka ili kuanzisha kampuni yake mwenyewe, na nafasi yake itazibwa na Andrew Bocking, mwingine mkongwe wa miaka 10 kikosini.
Lakini si yeye tu. Clara Shih, mwanamama aliyekuwa akikiongoza kitengo cha 'Business AI' (AI ya Biashara), naye anaondoka. Shih alijiunga na Meta mwaka jana tu (Novemba 2024) kwa mbwembwe nyingi, lakini shinikizo la kazi likichangiwa na msiba wa ghafla wa baba yake mzazi, limemlazimu kuweka mpira kwapani. Nafasi yake inachukuliwa na Guy Rosen, ambaye amekuwa akisimamia masuala ya uadilifu (integrity) wa kampuni.
Kama hiyo haitoshi, wiki iliyopita kulizuka tetesi nzito kuwa Yann LeCun, anayeheshimika duniani kama mmoja wa "Mababa wa AI" na Mwanasayansi Mkuu wa Meta, naye yuko mbioni kufunga virago kwenda kuanzisha kampuni yake mpya (startup). Kuondoka kwa watu hawa wazito kwa mpigo ni ishara ya wazi kuwa "jikoni kumenuka."
Pesa, Hisa na Hofu ya Wawekezaji
Chanzo cha vurugu hizi zote ni kitu kimoja: Pesa.
Meta imekuwa ikimwaga fedha nyingi mno kwenye utafiti na miundombinu ya AI. Ingawa ripoti ya mapato ya robo ya tatu ilionyesha kampuni imeingiza faida nzuri, tangazo lao la kuwa "wataongeza matumizi makubwa zaidi" mwaka 2026 liliwaudhi wawekezaji. Wawekezaji wanahofu kuwa Mark Zuckerberg anacheza kamari na pesa zao kwenye miradi ya AI ambayo faida yake haionekani leo wala kesho.
Matokeo ya tangazo hilo yalikuwa mabaya: thamani ya hisa za Meta iliporomoka kwa takriban asilimia 20. Hii ni sawa na kupoteza mabilioni ya dola ndani ya muda mfupi. Wawekezaji wanataka kuona faida sasa, siyo ahadi za miaka kumi ijayo.
Mkakati Mpya: 'Safisha na Ujenge Upya'
Ili kupunguza kelele za wenye mali (wanahisa), Meta inaonekana kuchukua hatua kali. Kampuni hiyo imeamua kuachana na miradi mingine na kuelekeza nguvu zote kwenye maabara mpya inayoitwa 'Superintelligence Lab (MSL)' chini ya uongozi wa Alexandr Wang, Afisa Mkuu mpya wa AI.
Mkakati huu mpya unahitaji "damu mpya" na kuondoa "mafuta yasiyohitajika." Hii ndiyo sababu, mbali na mabosi hawa kuondoka, Meta hivi karibuni imewafuta kazi watafiti wa AI wapatao 600. Lengo ni kupunguza gharama za mishahara ili pesa hizo zielekezwe kwenye kununua vifaa (chips) na kujenga seva kubwa zaidi.
Kwa wafanyakazi waliobaki, hali ni ya wasiwasi na shinikizo la kazi limeongezeka maradufu. Wanatakiwa kuthibitisha kuwa miradi wanayofanya inaingiza pesa au inasaidia AI kukua haraka, vinginevyo, mlango wa kutokea uko wazi. Kwa Watanzania tunaotumia mitandao hii kufanya biashara au kupata habari, mabadiliko haya yanaweza kuleta huduma mpya za AI zenye nguvu zaidi, lakini kwa gharama ya ajira na utulivu ndani ya Meta.