Shirika la Anga za Juu la Marekani (NASA) limetangaza mpango wa dharura na wa kimkakati wa kujenga kinu cha nyuklia katika Mwezi ifikapo mwaka 2030. Lengo kuu ni kuzalisha nishati ya umeme itakayotumika katika kituo cha kudumu cha binadamu wanachopanga kukijenga huko, lakini pia, hatua hii inachukuliwa kama harakati ya kuwahi na kuwazidi kete washindani wao wakuu, China na Urusi.
Wazo la kujenga kinu cha nyuklia Mwezini si jipya, lakini tangazo hili la NASA linaashiria kuanza rasmi kwa mbio mpya za anga za juu za karne ya 21, ambapo nishati na udhibiti wa maeneo muhimu Mwezini ndio zawadi kuu.
Mashindano ya Kijiografia na Kisiasa
Chanzo kikuu cha kasi hii ya ghafla ya Marekani ni mpango wa pamoja wa China na Urusi, ambao walitangaza kuwa wanakusudia kujenga kituo chao cha nishati ya nyuklia Mwezini ifikapo mwaka 2035. Kuna hofu kwamba nchi itakayotangulia kujenga miundombinu yake muhimu, itaweza kutangaza "eneo salama" (safety zone) kuzunguka kituo chake.
Chini ya Mkataba wa Artemis wa mwaka 2020 unaoongozwa na NASA, nchi zinaruhusiwa kuweka maeneo salama ili kulinda vifaa vyao na kuzuia mwingiliano hatari na shughuli za nchi nyingine. Hivyo, Marekani ina hofu kuwa inaweza kuchelewa na kujikuta imezuiwa kufanya shughuli zake katika maeneo muhimu Mwezini endapo China na Urusi zitatangulia.
Kaimu Mkuu wa NASA, Sean Duffy, alisema hatua za haraka zinahitajika ili kuimarisha usalama wa taifa na kuhakikisha Marekani inapata maeneo ya kufanyia kazi Mwezini. Amesema atamteua mkuu wa mradi huu ndani ya siku 30, na kutoa zabuni kwa makampuni binafsi ndani ya siku 60. Lengo ni kuwa na kinu chenye uwezo wa kuzalisha umeme wa kilowati 100 ifikapo 2030.
Kwa Nini Nishati ya Nyuklia Inahitajika Mwezini?
Siku moja kamili Mwezini ni sawa na siku 29.5 za Dunia. Hii inamaanisha kuna takriban wiki mbili za mchana mfululizo, na kisha wiki mbili za usiku na giza totoro. Kutokana na giza hili la muda mrefu, kutegemea nishati ya jua (solar power) pekee kwa ajili ya kituo cha kudumu cha binadamu si jambo la uhakika. Wanasayansi wanaamini kuwa kinu kidogo cha nyuklia ndiyo njia bora zaidi ya kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na endelevu.
Je, Mpango Huu Unawezekana?
Baadhi ya wataalamu, kama Profesa Lionel Wilson wa Chuo Kikuu cha Lancaster nchini Uingereza, wamesema kuwa kufikisha kinu cha nyuklia Mwezini ifikapo 2030 "inawezekana kiteknolojia."
Hata hivyo, kuna changamoto kubwa. Utawala wa Rais Trump unaripotiwa kufikiria kupunguza bajeti ya NASA, jambo linalofanya mpango huu wa gharama kubwa uonekane kuwa mgumu kutekelezeka. Hata ufadhili wa mpango mkuu wa Artemis, unaohusika na kupeleka watu na vifaa Mwezini, bado hauna uhakika.
Wakati huo huo, baadhi ya wanasayansi wameonyesha wasiwasi wao kuwa mbio hizi mpya za anga za juu zinaendeshwa zaidi na siasa za kijiografia na maslahi ya kitaifa badala ya lengo kuu la uchunguzi wa kisayansi kwa manufaa ya binadamu wote.