Nchini Marekani, mjadala mkali wa kimaadili umezuka kufuatia kampuni moja ya kiteknolojia kuanza kutoa huduma ya kibiashara inayowaruhusu wazazi kuchambua vinasaba vya vijusi (embryos) vilivyotungwa maabara na kuchagua kipi cha kupandikiza tumboni, kwa lengo la kupata mtoto ambaye wanaamini atakuwa na afya bora zaidi.
Kampuni hiyo, inayojulikana kama 'Orchid Health', imezindua huduma inayodai kuchanganua vinasaba vya kijusi na kutoa alama za hatari ya kupata magonjwa zaidi ya 1,200, yakiwemo kichaa (schizophrenia), kusahau (dementia), na unene uliokithiri. Wazazi wanaotumia huduma hii wanaweza kuona ni kijusi kipi kina "alama za chini" za hatari na hivyo kukichagua kwa ajili ya kuendeleza ujauzito.
Mwanzilishi wa kampuni hiyo, Noor Siddiqui, anasisitiza kuwa anataka kuunda "kizazi kinachoweza kuepuka magonjwa," akidai kuwa zama zimefika ambapo ngono ni kwa ajili ya starehe, lakini uzazi unafanywa kwa kutumia data. Yeye mwenyewe amepanga kutumia teknolojia hii kupata watoto wanne. Hata hivyo, huduma hii si ya bei rahisi. Gharama yake ni Dola za Marekani 20,000 (takriban Shilingi milioni 52) kwa kila mzunguko mmoja wa utungishaji maabara (IVF), na Dola 2,500 za ziada (takriban Shilingi milioni 6.5) kwa kila kijusi kinachofanyiwa uchambuzi. Hii inaifanya huduma hii kuwa ya matajiri pekee, na miongoni mwa wateja wake anatajwa kuwa ni Shivon Zilis, mama wa watoto wa bilionea Elon Musk.
Hata hivyo, wanasayansi na wataalamu wa maadili wameibua maswali mazito kuhusu usahihi na usalama wa teknolojia hii. Profesa Svetlana Yatsenko wa Chuo Kikuu cha Stanford anaonya kuwa madai ya kuchambua vinasaba vyote bilioni 3 vya binadamu kutoka kwenye seli tano tu za kijusi ni hatari. Anasema, "Mchakato wa kusoma vinasaba vyote kutoka kwenye seli chache hivyo unaweza kuwa na makosa mengi," akisisitiza kuwa ni hatari sana kutoa uhakika kuhusu uwepo au kutokuwepo kwa jeni fulani.
Pia, wanasayansi wengine wanasema mfumo wa "alama za hatari" unaotumiwa na kampuni hiyo hauna msingi thabiti wa kisayansi katika kutabiri magonjwa. Chama cha Madaktari wa Uzazi cha Marekani kimeeleza wasiwasi wake mkubwa, kikisema, "Teknolojia kama hizi zinavuka mipaka ya utabiri na zinaingia kwenye kuendesha na kubadilisha mustakabali wa vijusi vya binadamu."
Wasiwasi unaongezeka zaidi kutokana na kuibuka kwa makampuni mengine yenye mipango mikali zaidi. Kampuni nyingine iitwayo 'Bootstrap Bio' inatengeneza teknolojia ya kubadilisha moja kwa moja DNA ya kijusi (gene editing), badala ya kuchagua tu. Teknolojia hii, ikifanikiwa, mabadiliko yatakayofanywa yatarithishwa kwa vizazi vyote vijavyo milele. Kutokana na sheria kali za Marekani, kampuni hiyo imepanga kufanyia majaribio yake ya kitabibu nchini Honduras ifikapo mwaka 2026.
Wataalamu wa maadili wanaonya juu ya hatari ya zama za "watoto wa kubuniwa." Profesa Lori Zoloth wa Chuo Kikuu cha Chicago anasema, "Jaribio la kuwaunganisha watoto kama vile ni vifaa ni mtazamo hatari." Huku Profesa Hank Greely wa Stanford akiongeza, "Hakuna anayejua nini hasa kitamtokea mtoto aliyebadilishwa vinasaba." Mnamo mwezi Mei mwaka huu, jumuiya ya wanasayansi duniani ilipendekeza kusitishwa kwa angalau miaka 10 kwa majaribio yote ya kubadilisha vinasaba vya uzazi wa binadamu.