Mambo yameharibika ndani ya himaya ya Apple. Kampuni hiyo ambayo kwa miongo kadhaa imekuwa ikisifika kama "mwamba usiotingishika" wa Silicon Valley kwa utulivu wa viongozi wake, sasa inapitia kipindi kigumu zaidi cha mabadiliko ya uongozi kuwahi kutokea. Wiki iliyopita pekee imeshuhudia vigogo wanne wa ngazi za juu wakitangaza kuondoka, huku hofu ikitanda juu ya mustakabali wa teknolojia ya kampuni hiyo.
Ripoti za Bloomberg zimethibitisha kuwa "kuvuja kwa ubongo" (brain drain) ndani ya Apple sasa kumefikia kiwango cha hatari, huku washindani kama Meta (Facebook) na OpenAI wakinufaika na mtafaruku huo.
Wiki ya Machozi: Vigogo Wanne Waaga
Ndani ya siku saba tu, ofisi za Apple zimeshuhudia barua nne nzito za kujiuzulu kutoka kwa Makamu wa Rais (VPs) wa vitengo nyeti:
- John Giannandrea (Mkuu wa AI): Aliondoka tarehe 1 baada ya kushindwa kuifikisha 'Siri' kwenye viwango vya kisasa na kuchelewesha maboresho yake kwa mwaka mzima.
- Alan Dye (Mkuu wa Ubunifu): "Mchoraji" wa sura ya iPhone na Apple Watch ametimkia kwa wapinzani, Meta, kuongoza kitengo cha Reality Labs.
- Kate Adams (Mwanasheria Mkuu): Mkuu wa kitengo cha sheria naye ametangaza kung'atuka.
- Lisa Jackson (Mkuu wa Sera na Mazingira): Sura ya Apple kwenye masuala ya mazingira nayo imejiondoa.
Mshtuko Mkubwa: 'Baba wa Apple Silicon' Kutaka Kuondoka
Hata hivyo, habari iliyoshitua zaidi ni tetesi kuwa Johny Srouji, Makamu wa Rais wa Teknolojia ya Vifaa (Hardware Technologies), anafikiria kuondoka.
Srouji anatajwa kama "Apple Silicon God" (Mungu wa Chipu za Apple). Yeye ndiye ubongo nyuma ya chipu za M1, M2, na M3 ambazo zimeifanya kompyuta za Mac kuwa tishio duniani. Kuondoka kwake kunatajwa kama pigo takatifu litakaloacha pengo kubwa kwenye ramani ya teknolojia ya Apple, kwani yeye ndiye injini ya ubunifu wa ndani. Inasemekana tayari amewadokezea wenzake kuwa anatafuta changamoto mpya nje ya Apple.
Kwanini Wanakimbia?
Wachambuzi wa masuala ya teknolojia wanasema kuna sababu kuu mbili:
- Kufeli kwenye AI: Apple imeonekana kuzidiwa kete na Google, OpenAI, na Meta kwenye ulimwengu wa Akili Mnemba (AI). Wataalamu wengi wa Apple wamekatishwa tamaa na hatua ya kampuni kutegemea mifumo ya nje (kama Google Gemini) badala ya kuendeleza ya kwao, jambo lililosababisha wahandisi wengi kukimbilia Meta.
- Ukame wa Ubunifu: Wataalamu wanadai Apple haijatoa bidhaa mpya ya "maajabu" (New Product Category) kwa miaka 10 iliyopita ambayo imefanikiwa kama iPhone. Mradi wa gari ulifutwa, na miwani ya Vision Pro bado haijashika soko vizuri.
Afya ya Tim Cook na Mrithi wake
Mbali na kuondoka kwa wasaidizi wake, Mkurugenzi Mtendaji Tim Cook naye amemulikwa. Kumekuwa na uvumi juu ya afya yake baada ya kuonekana akitetemeka mikono, ingawa wasaidizi wake wamekanusha vikali kuwa anaumwa.
Hata hivyo, kwa kuwa viongozi wengi wako katika umri wa miaka 60, mabadiliko haya yanaonekana kama "Mabadiliko ya Kizazi" (Generational Shift).
- Jeff Williams (COO) na Luca Maestri (CFO) tayari wamo mbioni kustaafu.
- John Ternus, Mkuu wa Uhandisi wa Vifaa, sasa anatajwa kwa nguvu kama mrithi (Successor) wa Tim Cook. Ternus amepewa jukumu jipya la kusimamia miradi ya siku zijazo kama Roboti na Miwani Mahiri.
Mikakati Mipya
Ili kuziba mapengo, Apple imempandisha Craig Federighi (Mkuu wa Software) kusimamia pia kitengo cha AI ili kuleta utulivu. Hata hivyo, swali linabaki: Je, Apple itaweza kushindana na kasi ya AI ikiwa "Wabunifu" na "Wahandisi" wake wakuu wote wanakimbia?
Kwa watumiaji wa bidhaa za Apple Tanzania, hii inaweza kumaanisha kuchelewa kwa teknolojia mpya au mabadiliko makubwa katika bidhaa zijazo kama iPhone za kukunja (Foldable) au roboti za nyumbani.