Meta (Facebook) Yageuka 'TANESCO', Yaingia Rasmi Kwenye Biashara ya Kuuza na Kununua Umeme

it | Mon Nov 24 2025


Meta (Facebook) Yageuka 'TANESCO', Yaingia Rasmi Kwenye Biashara ya Kuuza na Kununua Umeme

Katika kile kinachoonekana kama mabadiliko makubwa ya kibiashara, kampuni ya Meta, ambayo ni mmiliki wa mitandao pendwa nchini Tanzania ya Facebook, Instagram, na WhatsApp, imeamua "kujilipua" na kuingia kwenye soko la kuzalisha na kuuza umeme. Hatua hii inakuja wakati ambapo kiu ya nishati kwa ajili ya kuendesha mifumo ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI) inazidi kuwa kubwa, kiasi cha kutishia projesheni za kawaida za nishati duniani.


Kwa lugha nyepesi, ni kama vile mmiliki wa kiwanda kikubwa aamue kujenga bwawa lake la umeme badala ya kusubiri huduma kutoka TANESCO, akihofia kuwa gridi ya taifa haitaweza kuhimili mashine zake mpya.


Facebook Yataka Umeme wa Uhakika


Ripoti kutoka shirika la habari la Bloomberg zinasema kuwa Meta imetangaza mkakati mpya wa kuingia mikataba ya muda mrefu ya ununuzi wa umeme (Long-term Power Purchase Agreements). Lengo sio tu kununua umeme kama tunavyonunua LUKU, bali ni kuwekeza kwenye ujenzi wa mitambo mipya ya kuzalisha nishati ili kuhakikisha 'Data Centers' (Vituo vya Data) zao hazikwami.


Urvi Parekh, Mkuu wa Nishati Duniani wa Meta, ameeleza kwa uwazi kuwa kampuni hiyo haiwezi tena kukaa pembeni na kusubiri. "Wazalishaji wa umeme wanataka kuona watumiaji wanabeba dhamana ya kweli. Tusipopaza sauti na kuweka pesa mezani, ujenzi wa vituo vipya vya umeme utakuwa wa kusuasua," alisisitiza Parekh.


Hii inatokana na ukweli kwamba makampuni ya kuzalisha umeme yanaogopa kuwekeza mabilioni kwenye mitambo mipya bila kuwa na uhakika wa soko (Guaranteed Market). Meta sasa inakuja kama "mdhamini" anayesema, "Jengeni, sisi tutanunua."


Vita ya Miamba: Microsoft na Google Nao Wamo


Meta haiko peke yake katika vita hii ya kusaka nishati. Vigogo wengine wa teknolojia kama Microsoft (MS) na Google nao wamegeuka kuwa 'madalali' wa nishati. Imeripotiwa kuwa Microsoft tayari imeanza kuwekeza kwenye miradi ya nishati safi na imepata vibali vya kuuza umeme wa ziada watakaouzalisha. Hii ni sawa na kusema kampuni ya kompyuta sasa inafanya kazi za shirika la umeme.


Hali ni mbaya kiasi kwamba mradi mmoja tu wa kituo cha data cha Meta huko Louisiana, Marekani, unahitaji umeme mwingi kiasi cha kulazimisha kampuni ya nishati ya Entergy kujenga mitambo mitatu mipya ya gesi ili kukidhi mahitaji hayo.


Mkakati wa "Kuuza na Kununua"


Tofauti na watumiaji wa kawaida, Meta inapanga kuwa na uwezo wa kuuza umeme huo pia. Mkakati wao ni kuingia mikataba mikubwa, na ikitokea wamenunua umeme mwingi kuliko mahitaji yao ya siku hiyo, watauuza kwenye soko la jumla (wholesale market) ili kupunguza hasara. Hii ni mbinu ya kijanja ya kibiashara inayohakikisha hawapotezi pesa hata senti moja.


Mchambuzi kutoka kampuni ya Wood Mackenzie, Ben Hertz-Shargel, anasema mipaka kati ya mtumiaji na mzalishaji inafutika. "Sasa hivi, watumiaji wakubwa ndio lazima waingilie kati kuhakikisha umeme unazalishwa," alisema.


Maoni ya Zuckerberg: "Bora Tuwekeze Kuliko Kukwama"


Mwanzilishi wa Meta, Mark Zuckerberg, amekaririwa mara kadhaa mwaka huu akisisitiza kuwa hatari kubwa kwa kampuni yake si kupoteza pesa kwenye uwekezaji wa nishati, bali ni kukwama kukuza teknolojia ya AI kwa sababu ya ukosefu wa umeme.


Zuckerberg anaamini kuwa ili kufikia hatua ya 'Superintelligence' (Akili Mnemba yenye uwezo uliopitiliza), ulimwengu unahitaji nishati mara dufu ya iliyopo sasa. Hivyo, Meta imeamua kuanza na masoko ya nishati ya PJM (Marekani Mashariki na Kati) na MISO (Marekani ya Kati), maeneo ambayo yana changamoto ya kasi ndogo ya ujenzi wa miundombinu.


Hatua hii ya Meta ni funzo kubwa kwa mataifa yanayoendelea kama Tanzania, ikionyesha kuwa katika uchumi wa kidijitali, umeme si nishati tu ya kuwasha taa, bali ni "damu" inayoendesha ubongo wa teknolojia ya kesho.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.