Kuna tetesi kubwa zinazotikisa ulimwengu wa teknolojia huko Silicon Valley, Marekani. Kampuni ya Apple, watengenezaji wa simu maarufu za iPhone, inaripotiwa kuanza mchakato wa kimya kimya wa kumpata mrithi wa kiti cha Uafisa Mtendaji Mkuu (CEO), huku kiongozi wao wa sasa, Tim Cook, akijiandaa kustaafu mwaka ujao.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya kuaminika kama gazeti la Financial Times, Bodi ya Wakurugenzi ya Apple na viongozi waandamizi wameanza rasmi mchakato wa kumtafuta atakayechukua nafasi ya Cook, ambaye amedumu kwenye kiti hicho kwa zaidi ya miaka 14.
Enzi ya Tim Cook: Pesa Ndefu, Akili Mnemba (AI) Dhaifu
Tim Cook, mwenye umri wa miaka 65 sasa, alichukua wadhifa huo mzito mwaka 2011 baada ya kifo cha mwanzilishi mwenza wa kampuni hiyo, gwiji Steve Jobs. Tofauti na Jobs aliyekuwa mbunifu wa bidhaa, Cook alijikita zaidi katika uendeshaji na biashara. Na kwa hakika, alifanya maajabu ya kifedha.
Wakati alipokabidhiwa kijiti, thamani ya soko ya Apple ilikuwa takriban Dola bilioni 350. Leo, chini ya uongozi wake, kampuni hiyo imevimba na kufikia thamani ya kutisha ya Dola trilioni 4 (sawa na mabilioni ya mabilioni ya Shilingi za Kitanzania), na kuifanya kuwa moja ya kampuni tajiri zaidi katika historia ya binadamu.
Hata hivyo, mafanikio haya makubwa ya kifedha yamegubikwa na kivuli kimoja kikubwa: kasi ndogo kwenye mapinduzi ya Akili Mnemba (AI). Wakati makampuni pinzani kama Nvidia, Microsoft, na Google yanakimbia na kujitanua kwenye teknolojia ya AI, Apple imeonekana ikiburura miguu. Hali hii imeifanya Apple ionekane zaidi kama kampuni ya 'bidhaa za anasa' (consumer goods) badala ya kuwa kiongozi wa teknolojia.
Wakati Sahihi wa Kuondoka
Kuondoka kwa Cook hakuhusiani na utendaji mbovu wa hivi karibuni. Kinyume chake, Apple inatarajia kupiga pesa nyingi zaidi mwishoni mwa mwaka huu kutokana na mauzo mazuri ya simu mpya ya iPhone 17.
Inatarajiwa kwamba Cook atatangaza kustaafu kwake rasmi mwakani 2026, mara tu baada ya kutangaza matokeo ya robo ya kwanza ya mwaka (mwishoni mwa Januari). Mpango huu utatoa nafasi kwa Mkurugenzi mpya kuizoea kampuni kabla ya matukio makubwa ya mwaka, ikiwemo mkutano mkuu wa watengenezaji programu (WWDC) mwezi Juni na uzinduzi wa iPhone mpya mwezi Septemba.
Mrithi Anayetajwa: Nani Huyu John Ternus?
Ingawa uamuzi wa mwisho bado haujafanywa, jina linalopewa kipaumbele zaidi kumrithi Tim Cook ni John Ternus, ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais Mwandamizi anayesimamia Uhandisi wa Vifaa (Hardware Engineering).
Dalili za mabadiliko haya zilianza kuonekana mapema mwaka huu. Watu wa karibu wa Tim Cook wameanza kupunguzwa. Afisa Mkuu wa Fedha (CFO), Luca Maestri, aling'atuka mapema mwaka huu, na 'mtu wa mkono' wa Cook, Afisa Mkuu wa Uendeshaji (COO) Jeff Williams, naye aliondoka mwezi Julai.
Kuteuliwa kwa Ternus, ambaye ni mtaalamu wa bidhaa na vifaa, kunaonekana kama mbinu ya kimkakati ya Apple. Inaashiria kuwa kampuni hiyo sasa inataka kuweka nguvu zake zote kwenye sekta ambazo Tim Cook alichelewa kuzishika: vifaa vya Akili Mnemba (AI devices) na Roboti (Robotics). Hii ni katika harakati za Apple kujaribu kurudisha hadhi yake kama wavumbuzi wakuu wa teknolojia duniani, badala ya kuwa wauzaji wa simu za gharama pekee.
Tim Cook mwenyewe aliwahi kudokeza mwezi Novemba kwenye mahojiano ya 'podcast' kwamba anapendelea mrithi wake atoke ndani ya kampuni hiyo, akisisitiza kuwa Apple "ina mpango wa kina sana wa urithi."