Enzi ya Tim Cook Apple Kuelekea Ukingoni? Mrithi Wake Anatafutwa Kimya Kimya

international | Sat Oct 11 2025


Enzi ya Tim Cook Apple Kuelekea Ukingoni? Mrithi Wake Anatafutwa Kimya Kimya

Wakati Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni kubwa ya teknolojia duniani, Apple, Tim Cook, akikaribia kutimiza umri wa miaka 65 mnamo Novemba 1, tetesi na mijadala mizito imeanza ndani ya kampuni hiyo kuhusu nani atarithi kiti chake. Ingawa Cook mwenyewe hajatangaza rasmi mpango wowote wa kustaafu, vyanzo vya habari vinaarifu kuwa Apple inafanya maandalizi ya kimyakimya kuhakikisha mabadiliko ya uongozi yanafanyika bila kuathiri utendaji wa kampuni.


Tangu alipochukua wadhifa huo kutoka kwa mwanzilishi mwenza wa Apple, Steve Jobs, mwaka 2011, Tim Cook amekuwa na mafanikio ya kihistoria. Chini ya uongozi wake, thamani ya hisa za Apple imepanda kwa takriban mara 18, na kuifanya kuwa moja ya kampuni zenye thamani kubwa zaidi duniani. Wakati Jobs anakumbukwa kwa kuleta mapinduzi ya iPhone, Cook amesifiwa kwa kupanua himaya ya Apple kupitia huduma za kidijitali (subscriptions), vifaa vya kuvaliwa kama Apple Watch, na vifaa vya sauti (earbuds), na kuunda mfumo wa kipekee unaowafunga wateja wake.


Kwa mujibu wa ripoti kutoka shirika la habari la Bloomberg, jina linalotajwa kuwa na uzito mkubwa zaidi kumrithi Cook ni John Ternus, Makamu wa Rais anayesimamia uhandisi wa vifaa. Ternus, mwenye umri wa miaka 50, ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 ndani ya Apple, akiongoza usanifu na uhandisi wa bidhaa muhimu. Umri wake unatajwa kuwa faida kubwa, kwani unampa fursa ya kuiongoza kampuni kwa muongo mmoja ujao au zaidi, na hivyo kuleta mwendelezo thabiti wa uongozi.


Katika siku za hivi karibuni, Ternus ameanza kuonekana zaidi hadharani, akiongoza matukio muhimu kama uzinduzi wa ‘iPhone Air’ na kushiriki katika hafla za uzinduzi kwenye maduka ya Apple, hatua inayotafsiriwa kama kumuandaa kwa majukumu makubwa zaidi.


Hapo awali, Jeff Williams, aliyekuwa Afisa Mkuu wa Uendeshaji (COO), alionekana kama mrithi wa asili, lakini alijiuzulu mapema mwaka huu na anatarajiwa kustaafu kabisa mwishoni mwa mwaka. Kuondoka kwake kumeibua upya mjadala wa nani atavaa viatu vya Tim Cook. Majina mengine yanayotajwa kama warithi watarajiwa ni pamoja na Craig Federighi, anayeongoza idara ya programu (software), na Greg Joswiak, mkuu wa idara ya masoko.


Hadi sasa, Apple haijatoa taarifa yoyote rasmi kuhusu kustaafu kwa Cook au mchakato wa kumtafuta mrithi wake, lakini ni dhahiri kuwa kampuni hiyo ipo katika mchakato muhimu wa kupanga mustakabali wake wa uongozi.

I recommend this article.

You can participate in article recommendations up to 50 times within 24 hours.


0 comments


Messages unrelated about this certain topic may be deleted or restricted.

0/300
Loading...

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.