Vita ya kuwania vipaji vya hali ya juu katika bonde la teknolojia la Silicon Valley imechukua sura mpya na ya kusisimua. Kampuni ya Meta, inayomiliki mitandao pendwa ya Facebook, Instagram, na WhatsApp, imetoa "ngumi ya chembe" kwa mshindani wake mkuu, Apple Inc., baada ya kufanikiwa kumshawishi na kumsajili mmoja wa vigogo wake wakuu wa ubunifu, Alan Dye.
Tukio hili, lililoripotiwa na Bloomberg tarehe 3 Desemba, limepokelewa kama tetemeko ndani ya Apple Park, likiashiria mwendelezo wa kile wachambuzi wanakiita "kuvuja kwa akili" (Brain Drain) kutoka kwa watengenezaji hao wa iPhone kwenda kwa washindani wanaowekeza zaidi kwenye Akili Mnemba (AI).
Alan Dye: "Mchoraji" wa Sura ya iPhone
Alan Dye si mtu wa kawaida. Tangu alipojiunga na Apple mwaka 2006, amekuwa ndiye "injini" nyuma ya muonekano na utendaji wa vifaa ambavyo Watanzania wengi wanavitamani. Yeye ndiye aliyesimamia ubunifu wa iPhone X, saa za mkononi za Apple Watch, na kifaa kipya cha Vision Pro. Pia, aliongoza timu iliyosanifu mifumo ya uendeshaji ya iOS, macOS, na hata kiolesura kipya cha 'Liquid Glass' kilichozinduliwa majuzi.
Kuondoka kwake ni pigo kubwa, kwani Dye alikuwa akiongoza kitengo nyeti cha Human Interface Design. Ni kama vile timu ya mpira impoteze kiungo wake mchezeshaji wakati wa fainali.
Zuckerberg Amchekelea, Kazi Mpya Desemba 31
Mkurugenzi Mtendaji wa Meta, Mark Zuckerberg, ana kila sababu ya kutabasamu. Dye anatarajiwa kuanza kazi rasmi Meta tarehe 31 Desemba, usiku wa kuamkia Mwaka Mpya, akiwa na cheo kipya cha Afisa Mkuu wa Ubunifu (Chief Design Officer - CDO) wa studio mpya ya kubuni vifaa.
Jukumu lake kuu litakuwa kubuni muonekano wa kizazi kijacho cha Miwani ya AI (AI Glasses), Vifaa vya Uhalisia Pepe (VR Headsets), na vifaa vingine vya kuvaliwa (Wearables). Zuckerberg amesisitiza kuwa sasa "Akili (Intelligence) imekuwa malighafi mpya ya ubunifu," akiamini kuwa Dye ndiye mtu sahihi wa kuifanya teknolojia hiyoivaliwe na binadamu kwa urahisi na mvuto.
Apple Yajitetea, Yamteua Mkongwe Kuziba Pengo
Katika kujaribu kutuliza hofu ya wawekezaji na mashabiki, Apple imekiri kuondoka kwa Dye na haraka imemtangaza Stephen Lemay kuchukua nafasi hiyo. Lemay ni "mkongwe wa nyumbani" ambaye amekuwepo Apple tangu mwaka 1999 na ameshiriki katika ubunifu wa karibu kila kitu cha Apple.
Mkurugenzi wa Apple, Tim Cook, amemwagia sifa Lemay akisema: "Stephen amekuwa nguzo muhimu tangu 1999... Viwango vya ubunifu vya Apple havitateteleka."
Mfululizo wa 'Kuhama Kambi'
Hata hivyo, wadadisi wa mambo wanasema "moshi ukitoka, moto upo chini." Kuondoka kwa Dye kunaongeza orodha ndefu ya vigogo walioikimbia Apple hivi karibuni, akiwemo Afisa Uendeshaji Mkuu (COO) Jeff Williams, Mkuu wa AI John Giannandrea, na Mkuu wa Vifaa Dan Riccio.
Inaonekana kuna mvutano mkubwa ndani ya Apple, huku wataalamu wengi wakivutiwa na kasi ya makampuni kama Meta na OpenAI katika ulimwengu mpya wa AI, tofauti na Apple ambayo inaonekana kwenda kwa mwendo wa kinyonga katika eneo hilo.
Kwa sasa, macho yote yanasubiri kuona je, Alan Dye atafanikiwa kuigeuza Meta kuwa "Apple mpya" kwa upande wa ubunifu wa vifaa? Au Apple itaendelea kuwa mwamba hata bila 'wachoraji' wake wakuu?