Kampuni kubwa ya teknolojia duniani, Amazon, imethibitisha kuwa ipo katika harakati za kuinunua kampuni changa ya Akili Bandia (AI) iitwayo 'Bee', hatua inayoashiria ushindani mkali unaoibuka katika soko la vifaa vya kuvaliwa vinavyotumia AI. Hata hivyo, ununuzi huu umeibua wasiwasi mkubwa kuhusu usiri na usalama wa data za watumiaji, hasa ikizingatiwa historia ya Amazon ya kukiuka sheria za faragha.
Kampuni ya Bee, iliyoanzishwa na Maria de Lourdes Zollo, inatengeneza kifaa cha kuvaliwa mkononi kama bangili au saa, kinachofanana na Fitbit. Kifaa hiki kina uwezo wa kusikiliza na kurekodi sauti zote zinazomzunguka mtumiaji, isipokuwa kama atazima kipaza sauti mwenyewe. Lengo lake ni kurahisisha maisha kwa kusikiliza mazungumzo na kutengeneza vikumbusho (reminders) au orodha ya mambo ya kufanya (to-do lists) kiotomatiki. Bei yake ya rejareja ni Dola 49.99 (takriban Shilingi 130,000), bei ambayo ni nafuu sana ikilinganishwa na vifaa vingine vya aina hii.
Hatua hii ya Amazon inaonyesha kuwa inaingia rasmi kwenye mbio za kutengeneza vifaa vya AI vinavyovaliwa, soko ambalo linashirikisha makampuni mengine makubwa. Meta (kampuni mama ya Facebook) tayari inaweka AI kwenye miwani yake ya kisasa, OpenAI inatengeneza kifaa chake, na Apple inasemekana kutoa miwani yake yenye AI mwaka ujao.
Tatizo kubwa la vifaa hivi ni kwamba vinarekodi kila kitu, jambo linaloleta hatari kubwa ya kiusalama na ukiukwaji wa faragha. Swali la msingi ni: Nini kinatokea kwa sauti hizi zilizorekodiwa? Zinahifadhiwa wapi na zinatumikaje? Je, zinatumika kufundisha mifumo ya Akili Bandia?
Hadi sasa, Bee imekuwa na sera kali za kulinda faragha. Sera yao inasema mtumiaji anaweza kufuta data zake wakati wowote, na kwamba sauti zilizorekodiwa hazihifadhiwi wala kutumika kufundisha AI. Pia, wanasisitiza mtumiaji lazima apate idhini ya watu wengine kabla ya kurekodi mazungumzo yao. Kampuni hiyo ilikuwa inaendeleza teknolojia ya 'geofencing' itakayoruhusu kifaa kijizime chenyewe kulingana na eneo (kama vile ofisini au nyumbani) na vichujio vya maudhui ili kulinda zaidi faragha. Mpango wao wa kutumia AI inayofanya kazi ndani ya kifaa (on-device AI) badala ya kutuma data kwenye 'cloud' ulionekana kuwa salama zaidi.
Wasiwasi mkubwa unaibuka hapa: Je, sera hizi zote za ulinzi wa data zitaendelea kuwepo baada ya Amazon kukamilisha rasmi ununuzi wa kampuni ya Bee? Historia ya Amazon si safi katika eneo hili. Mnamo mwaka 2023, kampuni hiyo ilipigwa faini kubwa kwa kukiuka sheria za ulinzi wa data za watumiaji.
Afisa mmoja wa Amazon alithibitisha mpango wa kuinunua Bee lakini akasema dili bado halijakamilika. Aliongeza kuwa wafanyakazi wa Bee wamepewa ofa ya kujiunga na Amazon. Hali hii inawaacha wengi na maswali, wakingoja kuona iwapo teknolojia hii mpya itakuwa msaidizi wa maisha ya kila siku au chanzo kingine cha udukuzi wa taarifa binafsi.