Hajamaliza 'Form Six' Lakini ni Bosi OpenAI: Kijana Aliyepiga Chini Shule na Kutumia ChatGPT Kuwa 'Genius' wa Akili Mnemba

it | Tue Dec 02 2025


Hajamaliza 'Form Six' Lakini ni Bosi OpenAI: Kijana Aliyepiga Chini Shule na Kutumia ChatGPT Kuwa 'Genius' wa Akili Mnemba

Katika kile kinachoonekana kama "kuchana vyeti" na kuandika upya kanuni za mafanikio, kijana mmoja amewashangaza walimwengu kwa kupata moja ya kazi zinazotamaniwa zaidi duniani bila kuwa na shahada ya Chuo Kikuu. Gabriel Peterson, ambaye kwa sasa ni Mtafiti wa Akili Mnemba (AI) katika kampuni kubwa ya OpenAI (wamiliki wa ChatGPT), amefichua siri ya jinsi alivyotumia roboti ya ChatGPT kujifunza mambo magumu ambayo kwa kawaida hufundishwa kwa ngazi ya PhD.


Kisa hiki ni kengele ya kuamsha kwa vijana wa Kitanzania, kuanzia wanafunzi wa VETA hadi wale wa UDSM, kwamba katika dunia ya sasa, "Ujuzi ni Mali, Vyeti ni Mapambo."


Kutoka Kuacha Shule Hadi Silicon Valley


Peterson aliacha shule ya sekondari nchini Norway mwaka 2019. Kwa lugha ya kijiweni, tunaweza kusema "alipiga chini shule" kabla hata ya kumaliza 'Form Six'. Bila uzoefu wowote wa uhandisi, alijiunga na kampuni changa (startup) huko Stockholm, Uswidi.


Akiwa huko, alipewa jukumu la kutengeneza mfumo wa kupendekeza bidhaa (recommendation system) kwa ajili ya biashara za mtandaoni. Ili kutatua changamoto hiyo, alilazimika kujifunza kuandika kodi za kompyuta (coding) kwa lazima. Lakini tofauti na wanafunzi wa vyuo wanaokariri nadharia (theory) kwanza, Peterson alitumia njia ya "kujifunza kwa vitendo."


Siri ya Mafanikio: "Nifundishe Kama Mtoto wa Miaka 12"


Peterson anasema alitumia ChatGPT kama mwalimu wake binafsi (Private Tutor). Mbinu aliyotumia inajulikana kama 'Recursive Gap Filling' (Kujaza Mapengo kwa Kujirudia).


Mbinu hii inafanya kazi hivi:


  1. Anauliza ChatGPT imtengenezee mfumo au kodi ya programu fulani.
  2. Kodi hiyo ikileta hitilafu (bugs), anaomba ChatGPT imsaidie kurekebisha.
  3. Ili kuelewa kwanini kodi hiyo inafanya kazi, anamuuliza roboti maswali kama: "Nieleweshe dhana hii kama unamuelewesha mtoto wa miaka 12."


"Nilipoendelea kufanya hivi mara kwa mara, nilijikuta nikijaza mapengo ya elimu yangu. Ilifika mahali sikutumia tena njia hiyo kwa sababu nilikuwa nimeelewa msingi mzima wa kompyuta na 'Machine Learning' kuliko hata wale waliosoma darasani," alieleza Peterson kwenye mahojiano ya Podcast hivi karibuni.


Sasa, kijana huyu anashiriki katika kutengeneza mfumo mpya na wa kisasa wa 'Sora' wa OpenAI, unaotengeneza video kwa kutumia maandishi.


Vyuo Vikuu Vyapoteza 'Hati Miliki' ya Elimu


Kauli ya Peterson imekuja wakati mwafaka. Amesema wazi kuwa, "Vyuo Vikuu sio tena wamiliki pekee wa maarifa ya msingi. Ukiwa na ChatGPT, unaweza kupata elimu yoyote ya msingi unayotaka."


Anawashauri vijana kuzingatia MATOKEO badala ya SIFA (Vyeti). "Kampuni zinataka kutengeneza pesa. Ukionyesha kuwa una uwezo wa kuingiza pesa na unaweza kuandika kodi (coding), watakuajiri tu, hawajali umesoma wapi," alisisitiza.


Mabosi wa Teknolojia Waunga Mkono


Hata mabosi wakubwa wa teknolojia wanakubaliana na mtazamo huu. Mkurugenzi Mtendaji wa OpenAI, Sam Altman, ambaye naye aliacha chuo kikuu cha Stanford, amekaririwa akisema anawaonea wivu vijana wa sasa walioacha chuo (dropouts).


"Kuna fursa nyingi sana za kutengeneza vitu hivi sasa, uwanja waushindani umesawazishwa," alisema Altman.


Naye Alex Karp, Mkurugenzi wa kampuni ya ulinzi ya Palantir, ameenda mbali zaidi na kudai kuwa "Kila kitu unachofundishwa shuleni na vyuoni kuhusu jinsi dunia inavyoenda ni makosa." Kampuni yake imeanzisha programu maalum ya kuwapa ajira na mafunzo vijana waliomaliza sekondari na hawakwenda chuo.


Funzo kwa Kijana wa Kitanzania


Simulizi ya Peterson inatufundisha kuwa elimu haipatikani darasani pekee. Simu janja uliyonayo mkononi ina uwezo wa kukugeuza kuwa mtaalamu wa kiwango cha dunia kama utaitumia kujifunza badala ya kupiga umbea mtandaoni.


Kama kijana wa Norway ameweza kuacha shule na kuajiriwa na kampuni kubwa duniani kwa kutumia ChatGPT kujifunza, wewe unayesubiri ajira serikalini una kisingizio gani? Wakati umefika wa kutumia 'bundle' yako kuwekeza kwenye ubongo.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.