Msemo wa "Mteja ni Mfalme" umeonekana kuingia dosari huko Marekani na duniani kote kwa watumiaji wa mtandao wa ChatGPT. Hali ya hewa imechafuka ghafla baada ya kampuni ya OpenAI kuanza kufanyia majaribio kipengele kipya kinachowasukumizia watumiaji matangazo ya kupakua programu (Apps) katikati ya maongezi, jambo ambalo limepokewa kwa hasira kali, hasa na wale wanaolipia huduma hiyo pesa ndefu.
Fikiria umelipia king’amuzi chako kifurushi cha juu kabisa ili ufurahie mpira bila kero, halafu ghafla katikati ya mechi unaletewa tangazo la dawa ya meno lisilo na kichwa wala miguu. Hivyo ndivyo watumiaji wa ChatGPT wanavyohisi sasa.
Kisa cha Bwana Jin na App ya 'Peloton'
Sakata lilianza pale Bwana Yuchen Jin, mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Hyperbolic, alipoamua kumwaga povu kwenye mtandao wa X (zamani Twitter). Jin alilalamika kuwa wakati akiwa kwenye mazungumzo na ChatGPT kuhusu mambo ya kikazi, ghafla roboti hiyo ilimkatisha na kumpigia debe apakue App ya mazoezi inayoitwa 'Peloton'.
Jin alihoji kwa ukali: "Ninalipa Dola 200 (sawa na takriban Shilingi 540,000 za Kitanzania) kila mwezi kwa ajili ya kifurushi cha 'Pro', inakuwaje naletewa uchafu huu unaofanana na matangazo?" Picha (Screenshot) aliyoiweka ilisambaa kama moto wa kifuu, huku watumiaji wengine wakieleza kero zao. Mwingine alilalamika kuwa anatumia Apple Music, lakini ChatGPT inalazimisha kumpendekezea Spotify kila saa.
OpenAI Yajitetea: "Sio Matangazo, Ni Ushauri Tu"
Baada ya kelele kuwa nyingi, Daniel McCauley, kiongozi wa data pale OpenAI, alijitokeza kujaribu kuzima moto. Alidai kuwa hicho wanachokiona watumiaji "sio matangazo ya kulipiwa," bali ni kipengele kipya kinacholenga kumsaidia mtumiaji kugundua Apps nzuri.
"Hatufanyi hivi kwa ajili ya pesa," alijitetea McCauley. "Hata hivyo, tunakiri kuwa kupendekeza App isiyoendana na mazungumzo ni uzoefu mbaya (Bad UX), na tunalifanyia kazi hilo."
Msemaji wa OpenAI naye aliongeza kuwa lengo lao ni kufanya Apps zigundulike kiasili ndani ya mazungumzo, kama ilivyotangazwa mwezi Oktoba kwenye mpango wao wa 'ChatGPT Apps'. Lengo lao la muda mrefu ni kuifanya ChatGPT iwe kama "Soko Kuu" (App Store) ambapo unaweza kupata huduma za Booking.com, Canva, au Uber moja kwa moja bila kutoka kwenye chati.
Shida Iko Wapi?
Tatizo kubwa ambalo wataalamu wa teknolojia wanaliona ni "Uvamizi wa Faragha" na ukosefu wa uhuru.
- Mapendekezo Yasiyo na Mantiki: Roboti inapendekeza App ya 'gym' wakati watu wanajadili kodi za kompyuta. Hii inaonekana kama usumbufu.
- Hakuna Kitufe cha 'Zima': Mtumiaji hana uwezo wa kuzima (Opt-out) mapendekezo haya. Anaulazimishwa kuyaona hata kama hataki.
- Harufu ya Matangazo: Hata kama OpenAI wanasema siyo matangazo, kwa mtumiaji wa kawaida, kitu chochote kinachokuambia "Pakua hii," ni tangazo.
Wadadisi wanasema hatua hii inaweza kuharibu mkakati wa OpenAI wa kutaka kuwa badala ya Google Play Store au Apple Store. Ili watumiaji wakubali kutumia Apps ndani ya ChatGPT, lazima wajisikie huru na wasione kama wanasukumizwa bidhaa kinguvu.
Kwa sasa, majaribio haya yanafanyika katika nchi nyingi duniani isipokuwa Umoja wa Ulaya (EU) na Uingereza ambako sheria za kidijitali ni kali sana. Kwa watumiaji wa Tanzania, tujipange; huenda hivi karibuni tukiwa tunamuuliza ChatGPT kuhusu historia ya Mkwawa, atatupendekezea kupakua App ya mapishi!