Katika ulimwengu wa Akili Mnemba (AI), jina Ashish Vaswani lina heshima ya kipekee. Yeye ndiye mwandishi kiongozi wa ile ripoti maarufu ya utafiti iitwayo "Attention Is All You Need" (Transformer Paper) iliyochapishwa na Google, ambayo ndiyo msingi wa teknolojia zote za kisasa za AI tunazoziona leo kama ChatGPT na Gemini.
Baada ya ukimya wa miaka miwili tangu alipoanzisha kampuni yake mpya ya Essential AI, Vaswani amevunja ukimya kwa kishindo. Siku ya Alhamisi (Desemba 5), kampuni yake imezindua roboti yao ya kwanza iitwayo ‘Rnj-1’, ambayo imetajwa kuwa ndiyo bora zaidi duniani kwa ukubwa wake katika mifumo ya wazi (Open Source).
Kwa Heshima ya 'Mungu wa Hesabu'
Jina 'Rnj-1' limepewa kwa heshima ya mwanahisabati nguli wa India, Srinivasa Ramanujan. Hii ni ishara kuwa roboti hii imepikwa maalum kwa ajili ya kazi za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, na Hisabati (STEM) pamoja na uandishi wa kodi za kompyuta (Coding).
Huu ni mfumo mdogo wenye vigezo (parameters) bilioni 8 (8B), lakini unafanya mambo makubwa kuliko mifumo mikubwa. Essential AI inasema lengo lao ni "Kutoa teknolojia ya hadhi ya juu ya Marekani kwa njia ya wazi (Open Source) kwa dunia nzima."
Utendaji: Dogo Janja Aangusha Vigogo
Katika majaribio ya kimaabara (Benchmarks), 'Rnj-1' imeonyesha uwezo wa kushangaza:
- Hesabu na Coding: Imewapiku washindani wake wa karibu kama Qwen 3 8B (ya China) na Gemma 3 12B (ya Google) katika mitihani ya hisabati (AIME 2025).
- Kipimo cha Umahiri: Katika mtihani mgumu wa SuperGPQA unaopima uelewa wa kiwango cha Uzamili (Masters/PhD), Rnj-1 imefanya vizuri sana, ikizidiwa kidogo tu na mfumo mkubwa wa OpenAI (gpt-oss-20b).
- Ufanisi: Mfumo huu unatumia teknolojia ya "Global Self-Attention" inayouwezesha kusoma na kuelewa maneno 32,000 kwa wakati mmoja, ikimfanya awe mwepesi na makini.
Falsafa Mpya: "Kurudi Kwenye Misingi"
Vaswani na mwanzilishi mwenza, Niki Parmar (ambaye pia ni mwandishi wa Transformer paper), wamesema wameamua "kurudi kwenye misingi" (Back to basics). Badala ya kuhangaika na mbinu za urembo (post-training), wameekeza nguvu kwenye mafunzo ya awali (Pre-training) ili kujenga msingi imara.
Vaswani anaamini kuwa teknolojia hii haipaswi kumilikiwa na makampuni machache makubwa. "Maendeleo katika elimu na afya hayapaswi kukwamishwa na teknolojia zilizofungwa (Closed AI)," alisisitiza. Hii ndiyo sababu wameamua kutoa mfumo huu bure kwa wataalamu kuutumia na kuuboresha.
Neema kwa 'Silicon Dar'
Kwa wabunifu wa programu na wataalamu wa IT nchini Tanzania, hii ni habari njema. Kwa sababu 'Rnj-1' ni ndogo (8B) na ni Open Source, inaweza kupakuliwa na kuwekwa kwenye kompyuta za kawaida au seva ndogo bila gharama kubwa.
Hii inatoa fursa kwa vijana wa Kitanzania kutengeneza mifumo ya AI ya kiswahili, kusaidia wanafunzi hesabu, au kusaidia madaktari vijijini kwa kutumia akili ya 'Rnj-1' bila kutegemea intaneti ya bei ghali au kulipia leseni za makampuni makubwa.
Essential AI, ambayo imeshakusanya mtaji wa Dola milioni 64.8 (Takriban Shilingi Bilioni 175), inaonekana imedhamiria kuleta ushindani wa kweli kwa OpenAI na Google kwa kuwapa nguvu watu wa chini.