Bima Zageuka Mbogo: Kampuni Kubwa Zakataa Kulipa Hasara za 'Uongo' wa Akili Mnemba (AI)

it | Tue Nov 25 2025


Bima Zageuka Mbogo: Kampuni Kubwa Zakataa Kulipa Hasara za 'Uongo' wa Akili Mnemba (AI)

Wakati dunia ikishangilia mapinduzi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI), kumezuka kizaazaa kipya katika sekta ya fedha. Kampuni kubwa za bima duniani zimeanza mchakato wa "kuruka kimanga" na kukataa kulipa fidia kwa hasara yoyote itakayosababishwa na teknolojia hii. Hatua hii imekuja baada ya kuongezeka kwa matukio ambapo mifumo ya AI inatoa taarifa za uongo (hallucinations) au kufanya makosa yanayogharimu mabilioni ya fedha.


Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Financial Times, vigogo wa bima nchini Marekani kama AIG, Great American, na WR Berkley wako katika hatua za mwisho za kubadilisha mikataba yao. Lengo lao ni kuweka vipengele vipya ("vifungu vya kujitoa") vitakavyowakinga dhidi ya kulipa hasara zitokanazo na matumizi ya roboti hizi za kisasa.


Hofu ya "Sanduku la Giza"


Kampuni ya WR Berkley imewasilisha pendekezo kwa mamlaka za udhibiti ili kuruhusiwa kuweka kipengele kinachosema hawatahusika na "matumizi yoyote halisi au yanayodhaniwa ya AI." Hii inamaanisha kuwa, kama kampuni yako itatumia AI na kupata hasara, bima haitakutambua.


Nayo kampuni ya AIG imewaambia wadhibiti wa jimbo la Illinois kuwa teknolojia ya 'Generative AI' (kama ChatGPT) ni pana mno na ina hatari ambazo hazitabiriki. Dennis Bertram, mkuu wa bima ya mtandao kutoka kampuni ya Mosaic, amefafanua hofu hiyo kwa lugha nyepesi: "AI ni kama sanduku jeusi (black box). Hatujui inawaza nini au inapata wapi majibu yake, hivyo ni vigumu kuikatia bima."


Matukio ya 'Kasheshe' Yaliyogharimu Mabilioni


Uamuzi huu wa makampuni ya bima haujaja kwa bahati mbaya. Kuna matukio ya hivi karibuni ambayo yamewafanya mabosi wa bima kushika vichwa:


  1. Air Canada na Roboti Muongo: Shirika la ndege la Air Canada lilijikuta matatani baada ya roboti yao ya huduma kwa wateja (Chatbot) kumdanganya mteja kuhusu punguzo la nauli ambalo halikuwepo. Mahakama iliamua kuwa shirika hilo lazima limlipe mteja huyo kwa sababu "ahadi ya roboti ni ahadi ya kampuni."
  2. Hasara ya Trilioni za Kitanzania: Kampuni ya Wolf River Electric imeishtaki Google ikidai fidia ya Dola milioni 110 (sawa na takriban Shilingi Bilioni 297 za Kitanzania) baada ya mfumo wa 'AI Overview' wa Google kutoa taarifa za uongo zilizoharibu biashara yao.
  3. Wizi wa Sauti (Deepfake): Kampuni ya uhandisi ya Uingereza, Arup, ilipigwa 'cha juu' cha Dola milioni 25 (takriban Shilingi Bilioni 67.5 za Kitanzania) baada ya matapeli kutumia AI kuiga sauti na sura za wakurugenzi wao na kuamuru uhamisho wa fedha.


Hatari ya "Kiyama cha Pamoja"


Kevin Kalinich, mkuu wa kitengo cha mtandao katika kampuni ya Aon, anasema tatizo sio hasara ya kampuni moja. Tatizo ni "Systemic Risk" (Hatari ya Mfumo Mzima).


"Bima inaweza kulipa ikitokea kampuni moja imepata hasara ya Dola milioni 400 hadi 500 (sawa na Shilingi Trilioni 1 hadi 1.3). Lakini ikitokea mtoa huduma mkuu wa AI (kama OpenAI au Google) amefanya kosa la kiufundi, mamilioni ya kampuni duniani yataathirika kwa mpigo. Hakuna kampuni ya bima yenye pesa za kulipa dunia nzima kwa wakati mmoja," alisisitiza Kalinich.


Angalizo kwa Wafanyabiashara


Hali hii inaashiria mabadiliko makubwa katika ulinzi wa biashara. Wataalamu wa sheria, kama Aaron Le Marquer, wanaonya kuwa hivi karibuni tutashuhudia vita vikali mahakamani kati ya wafanyabiashara na kampuni za bima pindi majanga makubwa ya AI yatakapotokea.

Kwa wafanyabiashara wa Kitanzania wanaoanza kukumbatia teknolojia hii, huu ni ujumbe tosha: "Chunga mzigo wako." Kutegemea bima kukulindia biashara yako dhidi ya makosa ya kompyuta kunaweza kusiwe tena chaguo salama. Wakati teknolojia inarahisisha kazi, bado inabaki kuwa na hatari zake ambazo sasa hata wenye pesa (Bima) wanaogopa kuzigusa.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.