Utafiti mpya na wa kimataifa umetoa onyo kali, ukibainisha kuwa kumpa mtoto simu ya mkononi (smartphone) katika umri mdogo, hasa kabla ya kufikisha miaka 13, kuna uhusiano wa moja kwa moja na matatizo mabaya ya afya ya akili anapofikia umri wa ujana na utu uzima. Ugunduzi huu unatarajiwa kuchochea zaidi mjadala unaoendelea duniani kote kuhusu umuhimu wa kuweka sheria na kanuni za kudhibiti matumizi ya simu kwa watoto na vijana.
Utafiti huo uliofanywa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Sapien Labs, inayojihusisha na utafiti wa afya ya akili na ubongo, ulichapishwa mnamo tarehe 21 Julai katika jarida la kimataifa la 'Journal of Human Development and Capabilities'. Watafiti walikusanya data kutoka kwa zaidi ya vijana 100,000 wenye umri wa kati ya miaka 18 na 24 kutoka nchi mbalimbali duniani.
Matokeo yalikuwa ya wazi: vijana ambao walipata simu zao za kwanza kabla ya umri wa miaka 13 waliripoti kukabiliwa na changamoto nyingi za kiakili walipofikia umri wa miaka 18-24. Changamoto hizo ni pamoja na mawazo ya kutaka kujiua, kuongezeka kwa hasira na ukali, kushindwa kudhibiti hisia, na kupoteza hali ya kujithamini.
Ili kupima hali hii, watafiti walitumia kipimo kiitwacho 'Mind Health Quotient' (MHQ), ambacho alama zake huanzia -100 (afya duni zaidi) hadi +200 (afya bora zaidi). Mtu mwenye afya njema ya akili huwa na wastani wa alama 100. Matokeo yalionyesha kuwa kadri mtoto anavyopata simu mapema, ndivyo alama zake zinavyokuwa chini. Kwa mfano, kundi lililopata simu likiwa na umri wa miaka 5 lilikuwa na wastani wa alama 1 tu, huku kundi la waliopewa simu kabla ya miaka 13 likiwa na wastani wa alama 30. Hii inaashiria madhara makubwa ya kiafya.
Aidha, utafiti uligundua tofauti za kijinsia. Wasichana walioanza kutumia simu mapema walionyesha viwango vya chini vya kujithamini na uwezo mdogo wa kuhimili misukosuko ya kihisia. Kwa upande wa wavulana, walionyesha upungufu katika utulivu wa ndani na uwezo wa kuhisi hisia za wengine (empathy).
Watafiti wanasisitiza kuwa matumizi ya simu katika umri mdogo huweza kusababisha matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, unyanyasaji mtandaoni (cyberbullying), kukosa usingizi wa kutosha, na hata migogoro ndani ya familia. Hivyo, walitoa wito kwa serikali na makampuni kuchukua hatua madhubuti, kama vile kutoa elimu ya lazima kuhusu matumizi salama ya kidijitali, kuwawajibisha wamiliki wa mitandao ya kijamii, na kuweka vizuizi vya umri katika matumizi ya simu.
Dkt. Tara Thiagarajan, mwanasayansi mkuu wa Sapien Labs, alisema, "Ingawa utafiti huu hauthibitishi uhusiano wa moja kwa moja wa chanzo na athari, kusubiri tafiti zaidi huku tukichelewa kuchukua hatua za kinga ni hatari kubwa."
Vuguvugu la kudhibiti matumizi ya simu kwa watoto shuleni linaenea kwa kasi duniani. Nchi kama Ufaransa ilipiga marufuku matumizi ya simu mashuleni tangu mwaka 2018. Uholanzi, Italia, Uhispania na Brazil zimefuata na sheria kama hizo. Kwa mujibu wa UNESCO, hadi mwaka jana, nchi 79 duniani zilikuwa na sera za kupiga marufuku matumizi ya simu mashuleni, kuonyesha kuwa suala hili sasa linaingia katika hatua za kisheria. Hali hii inazua maswali muhimu kuhusu sera na miongozo inayohitajika nchini Tanzania ili kulinda afya ya akili ya kizazi kijacho dhidi ya athari za teknolojia.