Tajiri namba mbili duniani na mwanzilishi wa himaya ya Amazon, Jeff Bezos, ameamua kustaafu "kustaafu kwake." Baada ya kukaa pembeni ya uongozi wa moja kwa moja tangu mwaka 2021, Bezos ameamua kurudi kwenye kiti cha dereva (CEO), safari hii akiongoza kampuni mpya ya kiteknolojia yenye lengo la kubadilisha jinsi dunia inavyofanya kazi.
Habari zilizotikisa soko la hisa na teknolojia zinamtaja Bezos kuwa Afisa Mtendaji Mkuu Mwenza (Co-CEO) wa kampuni mpya inayoitwa 'Project Prometheus'. Hii si kampuni ya kubahatisha; imezinduliwa ikiwa na mtaji wa kuanzia wa kutisha wa Dola za Kimarekani bilioni 6.2. Kwa fedha za Kitanzania, kiasi hiki ni takriban Shilingi Trilioni 16.1! Ili kukupa picha kamili, pesa hii inakaribia nusu ya bajeti yote ya Serikali ya Tanzania kwa mwaka mzima, na imewekezwa kwenye kampuni moja tu changa.
Dhamira: 'Akili ya Vitu Vigumu' (Physical Intelligence)
Tofauti na kampuni kama OpenAI (ChatGPT) au Google zinazojikita zaidi kwenye akili ya lugha na maandishi, 'Project Prometheus' ina lengo tofauti na gumu zaidi. Wanataka kuunda "World Models" (Mifumo ya Ulimwengu) na "Physical Intelligence" (Akili ya Kimwili).
Lengo lao ni kufundisha Akili Mnemba (AI) jinsi ya kuelewa na kudhibiti vitu katika ulimwengu halisi—kama vile kusaidia roboti kujenga magari, kuunda ndege, au hata roketi za kwenda angani. Hii inaendana moja kwa moja na maslahi mengine ya Bezos, ikiwemo kampuni yake ya anga za juu ya Blue Origin na uwekezaji wake kwenye kampuni za roboti kama Figure AI.
Bezos anataka AI isiishie kwenye kompyuta tu, bali iingie viwandani na maabara ili kufanya majaribio ya kisayansi na kihandisi kwa kasi ambayo mwanadamu hawezi kuifikia. Kwa kutumia ulimwengu wa kidijitali (virtual environment) kufanya majaribio, wanatarajia kuleta mapinduzi katika sekta za ujenzi, udaktari, na usafirishaji.
Mshirika Wake ni Nani?
Katika safari hii, Bezos hayuko peke yake. Ameungana na Dkt. Vik Bajaj, mwanasayansi nguli aliyewahi kufanya kazi na mwanzilishi wa Google, Sergey Brin, katika kitengo maalum cha 'Google X'. Bajaj ana uzoefu mkubwa katika miradi migumu kama magari yanayojiendesha na teknolojia za kibayolojia.
Vita ya Vigogo Yapamba Moto
Kurejea kwa Bezos kwenye ulingo wa uongozi ni habari mbaya kwa washindani wake. Tayari kampuni hii imeanza kwa kishindo kwa "kuiba" wafanyakazi bora (vipanga) kutoka OpenAI, Google DeepMind, na Meta. Inasemekana tayari wana kikosi cha wataalamu takriban 100 waliobobea.
Gazeti la New York Times linachambua kuwa hatua hii inamuweka Bezos katikati ya vita ya teknolojia dhidi ya mahasimu wake wa zamani na wapya, kama Elon Musk (xAI/Tesla), Mark Zuckerberg (Meta), na Sundar Pichai (Google). Bezos ameamua kuwa hataki kuwa mtazamaji au mwekezaji wa pembeni tena; anataka kuwa uwanjani akiongoza mapambano ya kuunda mustakabali wa sayansi na teknolojia.