Dunia ya teknolojia inashuhudia "vita mpya" ambayo siyo ya kodi (code) pekee, bali ni vita ya nishati. Wakati vituo vya data (Data Centers) vya Akili Mnemba (AI) vikizidi kusambaa duniani kote, changamoto kubwa imekuwa ni wapi pa kupata umeme wa kutosha kuziendesha mashine hizo nzito. Katika hatua ya kihistoria, kampuni ya Google imetangaza kununua kampuni kubwa ya nishati safi, Intersect Power, kwa kiasi cha Dola Bilioni 4.75 (takriban Shilingi za Kitanzania Trilioni 12.8).
Hatua hii ya Google ni mkakati wa "kujitegemea kiumeme" (power internalization), ambapo badala ya kusubiri kununua umeme kutoka kwa makampuni mengine, sasa wanamiliki "vinu" vyao wenyewe.
Ukubwa wa Mradi: Mara 20 ya Bwawa la Hoover
Kupitia ununuzi huu, Google itapata udhibiti wa miradi ya nishati inayozalisha au inayopangwa kuzalisha kiasi cha Gigawati 10.8 (10.8 GW) ifikapo mwaka 2028. Ili upate picha ya ukubwa huu:
- Kiwango hiki ni zaidi ya mara 20 ya umeme unaozalishwa na Bwawa maarufu la Hoover nchini Marekani.
- Ni sawa na kusema Google inatengeneza himaya ya nishati itakayoweza kuwasha mamilioni ya nyumba, lakini safari hii umeme huo wote ni kwa ajili ya "ubongo" wa AI.
Kwanini Google Imeamua Kuwa "Mzalishaji wa Umeme"?
Kuna sababu kuu tatu zilizopelekea Google kufanya uwekezaji huu mkubwa:
- Uchovu wa Miundombinu: Miundombinu ya umeme nchini Marekani ni ya zamani na haiwezi kuhimili kasi ya ukuaji wa AI. Kwa kununua Intersect Power, Google inajihakikishia umeme wa uhakika bila kutegemea gridi ya taifa inayoyumba.
- Kuepuka Vikwazo vya Kisheria: Mara nyingi, makampuni ya huduma za umeme (utilities) huwa na ukiritimba. Google ikimiliki kampuni ya nishati, inapata urahisi wa kujenga vituo vya data popote inapotaka bila kusubiri ruhusa ndefu za kuunganishwa umeme.
- Mkakati wa 'Green Energy': Intersect Power imebobea kwenye nishati ya jua (solar) na mifumo ya kuhifadhi umeme kwenye betri (battery storage), hususan katika jimbo la Texas. Hii inaisaidia Google kupunguza uharibifu wa mazingira.
Changamoto ya Kimazingira: AI vs. Hewa ya Ukaa
Pamoja na uwekezaji huu kwenye nishati safi, Google inakabiliwa na mtihani mzito. Ripoti yao ya hivi karibuni (2024) ilionyesha kuwa kutokana na kuongezeka kwa vituo vya data vya AI, uzalishaji wao wa hewa ya ukaa (carbon emissions) uliongezeka kwa 48% ndani ya miaka mitano iliyopita.
Hii ina maana kwamba kadiri AI inavyokuwa na akili, ndivyo inavyozidi "kula" nishati na kuhatarisha malengo ya kidunia ya kutunza mazingira. Amazon na Microsoft nazo zipo kwenye mtego huohuo, zikihangaika kununua vinu vya nyuklia na mashamba ya upepo ili kuzinusuru AI zao.
Uchambuzi wa Mtaalamu: "Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni kubwa ya teknolojia kununua kampuni ya nishati moja kwa moja. Google sasa siyo kampuni ya intaneti tu, bali ni kampuni ya nishati," anasema Ben Hertz-Shargel wa Wood Mackenzie.