Biashara ya 'AI Agents' Yaanza Kusuasua? Microsoft Yadaiwa Kushusha Malengo ya Mauzo, Yenyewe Yakana Vikali

it | Fri Dec 05 2025


Biashara ya 'AI Agents' Yaanza Kusuasua? Microsoft Yadaiwa Kushusha Malengo ya Mauzo, Yenyewe Yakana Vikali

Kuna msemo wa wahenga usemao, "Kupanda mchongoma, kushuka ndio ngoma." Baada ya miezi kadhaa ya nderemo na vifijo kuhusu mapinduzi ya Akili Mnemba (AI), hali halisi ya soko imeanza kuuma. Kampuni kubwa ya teknolojia duniani, Microsoft (MS), imejikuta katikati ya kimbunga cha habari zinazodai kuwa imeamua kupunguza malengo yake ya mauzo kwa bidhaa za AI, baada ya makampuni mengi kusita kuzinunua kwa kasi iliyotarajiwa.


Ripoti hizi zimezua hofu mpya katika soko la hisa la Wall Street na kuibua mjadala mzito: Je, huu ndio mwisho wa fungate (honeymoon) ya AI, au ni kigugumizi cha muda tu?


Mauzo Hayapandi, Wafanyabiashara Wasita


Kwa mujibu wa ripoti ya kiuchunguzi kutoka mtandao wa The Information, vyanzo vya ndani kutoka timu ya mauzo ya Microsoft vimelalamika kuwa "mzigo hautoki." Imeelezwa kuwa Microsoft ilikuwa imeweka malengo makubwa ya kuuza huduma zake za "AI Agents" (Wasaidizi wa Kidijitali wanaofanya kazi otomatiki) kwa makampuni makubwa mwaka 2025.


Lengo lilikuwa kukuza matumizi ya jukwaa la kibiashara la ‘Foundry’ kwa asilimia 50. Hata hivyo, uhalisia umekuwa mchungu; inasemekana chini ya asilimia 20 ya wauzaji ndio wameweza kufikia malengo hayo. Kutokana na hali hiyo ngumu, inadaiwa kuwa mabosi wa MS wameamua kupunguza malengo hayo kwa nusu ili kuendana na hali halisi ya soko.


Kwanini Makampuni Yanaogopa AI?


Wataalamu wa uchumi wanasema kuna sababu kuu mbili zinazowafanya wakurugenzi wa makampuni kushika breki kununua teknolojia hizi:


  1. Hesabu Hazikai Sawa (ROI): Wafanyabiashara wanashindwa kuona faida ya haraka. Kulipa mabilioni kwa ajili ya AI wakati huoni kama inakupunguzia gharama au kukuongezea faida kwa uhakika, ni kama kununua "mbuzi kwenye gunia."
  2. Hofu ya Uongo (Hallucinations): Katika sekta nyeti kama Benki, Fedha, na Usalama, kosa dogo la AI kutoa taarifa za uongo linaweza kugharimu hasara ya trilioni au kesi mahakamani. Hakuna bosi anayetaka kuweka rehani kampuni yake kwa roboti ambalo linaweza "kudanganya."


Sio Microsoft Tu, Hata OpenAI Wanalia


Hali hii si kwa Microsoft pekee. Imeripotiwa kuwa hata wababe OpenAI wamelazimika kupunguza makadirio yao ya mapato yatokanayo na 'AI Agents' kwa kiasi cha Dola bilioni 26 (sawa na takriban Shilingi Trilioni 70.2 za Kitanzania) kwa miaka mitano ijayo.


Vigogo wengine kama Salesforce na Amazon (AWS) nao wameanza kutoa ofa na punguzo la bei ili kuwabembeleza wateja wajiunge, ishara kuwa soko limekuwa gumu.


Mfano halisi umetolewa kwa kampuni kubwa ya uwekezaji ya Carlyle Group. Walijaribu kutumia mfumo wa Copilot Studio wa Microsoft, lakini waligundua kuwa roboti hilo lilishindwa kuongea vizuri na programu zao nyingine, jambo lililowalazimu kupunguza matumizi.


Microsoft Yakanusha, Hisa Zayumba


Baada ya taarifa hizi kusambaa na kusababisha taharuki, Microsoft ilijitokeza haraka kukanusha. Msemaji wa kampuni hiyo alisema, "Hajapunguza kiwango cha mauzo (Quota) cha bidhaa zetu za AI... ripoti hizi zimeelewa vibaya muundo wetu wa mauzo."


Hata hivyo, wawekezaji hawakuelewa somo hilo haraka. Hisa za Microsoft ziliporomoka kwa asilimia 3 mara tu baada ya habari kutoka, kabla ya kuimarika kidogo na kufunga soko zikiwa chini kwa asilimia 1.7.


Hii ni kengele ya hatari kwa soko la teknolojia. Wawekezaji sasa wameanza kuhoji kwa ukali: "Tumemwaga matrilioni kwenye miundombinu ya AI, faida iko wapi?" Kwa wafanyabiashara wa Kitanzania, funzo ni kuwa makini na teknolojia mpya; isikimbilie kununua kila kinachometa, pima faida na hasara kwanza.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.