Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA), mojawapo ya taasisi za afya zenye ushawishi mkubwa zaidi duniani, imeanzisha matumizi ya Akili Mnemba (AI) ili kuharakisha mchakato wa kuidhinisha dawa na vifaa vya matibabu. Hata hivyo, badala ya kuwa suluhisho, teknolojia hiyo mpya imeanza kuleta matatizo makubwa, huku wafanyakazi wa ndani wakiielezea kama "teknolojia ambayo bado haijawa tayari."
Chanzo cha Tatizo
FDA imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya mlundikano mkubwa wa kazi na uchache wa wafanyakazi, hasa baada ya kupunguzwa kwa takriban asilimia 20 ya wafanyakazi wake mapema mwaka huu. Hali hii imechelewesha kuidhinishwa kwa dawa muhimu, hasa zile za magonjwa nadra, mchakato ambao unaweza kuchukua kuanzia miezi nane hadi miaka kadhaa.
Ili kutatua tatizo hili, mwezi Juni, FDA ilizindua roboti wa AI aitwaye 'ELSA' (Electronic Labeling and Submission Assistant). Lengo la ELSA lilikuwa ni kusaidia kurahisisha kazi za ofisini zinazojirudia, kama vile kufupisha nyaraka ndefu za maombi ya dawa, kulinganisha lebo za bidhaa, na kuainisha taarifa. Matarajio yalikuwa ni kupunguza kazi za siku kadhaa zifanyike ndani ya dakika chache.
AI Yaifeli FDA
Hata hivyo, baada ya kuanza kutumika, kasoro za ELSA zimejitokeza waziwazi. Watathmini wa FDA wanaotumia roboti huyo wamelalamika kuwa mara nyingi "anatoa majibu yasiyoelewa hata dhana za msingi." Mfumo umekuwa ukishindwa kupakia nyaraka au unashindwa kuwasiliana vizuri na mifumo mingine ya ndani.
Kasoro kubwa zaidi ni kwamba, kwa sababu za kiusalama, ELSA amezuiwa kuunganishwa na intaneti ya nje. Hii ina maana kuwa hana uwezo wa kupata tafiti za kisayansi za hivi karibuni au data mpya, jambo linalomfanya asiwe na manufaa katika kutathmini dawa mpya za kisasa. Ni kama daktari anayezuiwa kusoma majarida mapya ya kitabibu.
Zaidi ya hayo, kumekuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu uaminifu wa taarifa zake. Katika visa kadhaa, ELSA alipoulizwa kufupisha orodha ya matumizi yaliyoidhinishwa ya dawa fulani, alitoa majibu ambayo sehemu yalikuwa sahihi na sehemu kubwa yalikuwa ya uongo. Hii ni hatari kubwa, kwani endapo mtathmini wa kibinadamu ataamini muhtasari huo bila kusoma waraka halisi, anaweza kufanya uamuzi mbaya unaohatarisha maisha ya watu. Wafanyakazi wanasema, "Ili kuamini muhtasari wake, inabidi usome waraka halisi kwa umakini zaidi," jambo linalopoteza kabisa lengo la kuokoa muda.
Suluhisho ni Ushirikiano, Sio Uendeshaji Kamili
Wataalamu wanasema mfumo bora kwa sasa si kuipa AI kazi yote, bali ni ushirikiano kati ya binadamu na AI. Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Indiana ulionyesha kuwa mfumo ambapo AI inapendekeza maeneo yenye hatari kubwa na kisha mtaalamu wa kibinadamu anafanya maamuzi ya mwisho, unapunguza makosa kwa karibu asilimia 40 na pia unapunguza mzigo wa kazi kwa asilimia 43.
Ingawa FDA inasema huu ni mwanzo tu na kwamba AI ni chombo msaidizi, kisa cha ELSA ni funzo muhimu kwa mamlaka nyingine duniani, kama vile Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA). Funzo lenyewe ni kwamba, kukimbilia kutumia teknolojia ya AI katika maeneo muhimu kama afya ya umma bila majaribio ya kutosha na usimamizi madhubuti wa kibinadamu kunaweza kuleta hasara badala ya ufanisi.