Wakati ulimwengu ukiendelea kushangazwa na maajabu ya Akili Mnemba (AI) katika kurahisisha kazi, ripoti mpya ya uchunguzi imefichua ukweli wa kutisha unaojificha nyuma ya pazia. Njaa isiyo ya kawaida ya nishati na rasilimali zinazohitajika kuendesha teknolojia hii sasa inatishia kusababisha mgogoro wa kimataifa wa nishati na mazingira, huku mahitaji ya umeme yakifikia viwango ambavyo havijawahi kufikiriwa.
Ripoti kutoka chombo cha habari cha TruthDig imefichua memo ya ndani ya kampuni ya OpenAI, inayoongozwa na Sam Altman, ambayo inaweka wazi mipango yao ya siku zijazo. Kulingana na mpango huo, inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2033, OpenAI pekee itahitaji miundombinu ya kompyuta yenye uwezo wa kutumia umeme wa Gigawati 250 (GW).
Ili kuelewa ukubwa wa namba hii, ni lazima tuiweke katika muktadha. Kiasi hicho cha umeme (250 GW) ni sawa na, au hata kinazidi, kiasi chote cha umeme kinachotumiwa na taifa zima la India—nchi yenye idadi ya watu bilioni 1.5. Hiyo ni kampuni moja tu.
Wataalamu wanaonya kuwa uendeshaji wa mitambo ya kiwango hicho utazalisha hewa chafu ya ukaa (carbon emissions) kwa kiwango cha kutisha, kinachoweza kuwa mara mbili ya kile kinachozalishwa na kampuni kubwa ya mafuta ya ExxonMobil, ambayo kwa sasa ndiyo inayoongoza kwa uchafuzi wa mazingira duniani kwa sekta binafsi.
Mahesabu ya Vifaa Vinavyohitajika
Ili kufikia matumizi hayo ya umeme, OpenAI itahitaji kuwasha na kuendesha takriban 'chips' (GPU) za kisasa za Nvidia (aina ya GB300) zipatazo milioni 60.
Tatizo linaongezeka maradufu kwa sababu 'chips' hizi zina "maisha ya kiuchumi" ya miaka miwili tu; si kwa sababu zinaharibika, bali kwa sababu teknolojia mpya yenye nguvu zaidi inatoka na kufanya zilizopita zionekane zimepitwa na wakati. Hii ina maana kwamba OpenAI italazimika kununua 'chips' mpya zipatazo milioni 30 kila mwaka ili tu kuendeleza mfumo wake.
Wote Wako Kwenye Mbio Hizi
Shida hii si ya OpenAI pekee. Mpinzani wake mkuu, Elon Musk, kupitia kampuni yake ya xAI, naye ameweka lengo la kununua 'chips' za H100 zipatazo milioni 50 ifikapo mwaka 2030, akihitaji takriban Gigawati 5 za umeme wa ziada.
Ujenzi huu mkubwa wa vituo vya data (Data Centers) unaweka shinikizo ambalo halijawahi kuonekana kwenye gridi za taifa duniani kote. Hali hii inatishia kupandisha bei za umeme kwa watumiaji wa kawaida majumbani na kusababisha mgao wa umeme (power rationing) ili kukidhi mahitaji ya viwanda hivi vya kidijitali. Zaidi ya hayo, vituo hivi hutumia mabilioni ya lita za maji safi kwa ajili ya kupooza mitambo, jambo linalotishia vyanzo vya maji katika maeneo mengi.
Tatizo linaanzia Kwenye Kiwanda
Njaa ya rasilimali haianzi kwenye kituo cha data; inaanzia kwenye kiwanda kinachotengeneza 'chip' zenyewe. Kutokana na mahitaji haya makubwa, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, ujenzi wa viwanda vipya vya 'semiconductors' (fabs) 97 umeanza duniani kote.
Makampuni kama TSMC na Samsung yanajenga viwanda vikubwa vya kutisha. Kwa mfano, kiwanda kimoja tu cha TSMC kinachojengwa ('Fab 25') kinatarajiwa kutumia Gigawati 1 ya umeme (sawa na matumizi ya nyumba 750,000 nchini Taiwan). Pia, kitatumia tani 100,000 za maji KILA SIKU—kiasi hicho ni sawa na matumizi ya maji ya wakazi 196,000 wa jiji la Taichung kwa siku.
Vita vya nani atatawala AI sasa vimegeuka kuwa vita vya nani atatumia rasilimali chache za dunia (umeme na maji) kwa kasi zaidi, na kuweka sayari yetu katika hatari kubwa ya kimazingira.