Vita vya teknolojia ya Akili Mnemba (AI) vimeingia awamu mpya na ya kutisha. Siyo tena vita vya 'software' na nani ana mfumo bora wa lugha; sasa ni vita vya nani anadhibiti 'ubongo' halisi unaoendesha mifumo hiyo—yaani, 'chips' maalum za AI. Na katika hili, Microsoft (MS) wamefanya 'mchongo' wa kimkakati utakaowapa kicheko cha mbali, baada ya kufichuka kuwa wamepata ruhusa ya kutumia teknolojia ya OpenAI ya kutengeneza 'chip' zao wenyewe.
Mkurugenzi Mkuu wa Microsoft, Satya Nadella, amethibitisha jambo ambalo limekuwa likinong'onwa kwa muda. Kwenye mahojiano ya 'podcast' na mwandishi Dwarkesh Patel, Nadella alifunguka: "Wakati OpenAI wanapofanya uvumbuzi wowote katika kiwango cha mfumo (system level), sisi tunapata ufunguo wa kuingia na kuona kila kitu." Aliongeza, "Kwanza tutatekeleza kile walichokitengeneza, na baadaye tutakipanua zaidi."
Kauli hii ya 'kiwango cha mfumo' ndiyo habari kubwa. Inathibitisha kwa mara ya kwanza kwamba mpango wa siri wa OpenAI wa kujitengenezea 'chip' zao wenyewe (kwa ushirikiano na kampuni ya Broadcom) ni sehemu ya mkataba wao na Microsoft. Hili halikuwa limewahi kuwekwa wazi hapo kabla.
Mwezi uliopita, kampuni hizi mbili zilifanya marekebisho ya mkataba wao kufuatia mabadiliko ya kimuundo ya OpenAI. Mkataba huo uliipa Microsoft haki ya kutumia mifumo ya OpenAI hadi mwaka 2032 na kupata fursa ya kuona tafiti zao hadi 2030. Ingawa ilitajwa kuwa mkataba hautahusisha vifaa vya kielektroniki vya watumiaji (kama simu), haikuelezwa lolote kuhusu 'chip' maalum za AI.
Kwa nini hili ni jambo kubwa? Kwa miaka kadhaa sasa, Microsoft wamekuwa wakijaribu kutengeneza 'chip' zao wenyewe zinazoitwa 'Maia' na 'Cobalt', lakini ukweli ni kwamba wameachwa mbali sana na washindani wao. Wababe wengine kama Google (wana 'TPU' zao), Amazon (wana 'Trainium' na 'Inferentia'), na Meta (wana 'MTIA') wote tayari wanatumia 'chip' zao maalum walizojitengenezea wenyewe katika vituo vyao vya data. Hali hii inawapa faida ya kasi na kupunguza gharama kubwa za uendeshaji.
Microsoft, kwa kiasi kikubwa, bado wanamtegemea 'mchizi mmoja' tu: kampuni ya Nvidia, ambayo ndiyo inatawala soko la 'chip' za AI duniani. Utegemezi huu ni hatari kimkakati na unagharimu mabilioni ya dola. Kwa kupata teknolojia ya 'chip' za OpenAI, Microsoft wanapata njia ya mkato ya kuwafikia washindani wao kwa kasi zaidi.
Satya Nadella alisisitiza kuwa ushirikiano huu utaimarisha sana miundombinu yao ya AI. Alisema, "Mifumo ya AI inafanya kazi kwa ufanisi zaidi pale ambapo 'hardware' (chip), mtandao, 'model' (kama ChatGPT), na 'software' vinapofanya kazi pamoja kama kitu kimoja."
Na kuonyesha ukubwa wa mchezo huu, Nadella alidokeza habari nyingine kubwa: Mbali na kituo chao kipya kikubwa cha data 'Fairwater' kitakachoanza kazi mwaka kesho, tayari wanaanza ujenzi wa 'Fairwater 2'. Kituo hiki kipya kitajengwa kwa kuunganisha majengo kadhaa yatakayokuwa na mamia ya maelfu ya 'chip' mpya za Nvidia (GB200 na GB300) na kitatumia kiasi cha umeme cha zaidi ya Gigawati MBILI (2 GW)—kiasi cha kutosha kuendesha miji mikubwa. Mahitaji haya makubwa ya umeme ndiyo yanayowasukuma zaidi kutafuta 'chip' zao zenye ufanisi zaidi, na hapo ndipo teknolojia ya OpenAI inapoingia.