Afya ya kinywa, ikijumuisha fizi na meno, ina uhusiano wa karibu na ustawi wa ubongo wako kuliko unavyoweza kufikiria. Tatizo linaanzia pale ambapo kemikali za uvimbe (inflammation) pamoja na vimelea vidogo kama bakteria vilivyopo mdomoni vinapopenya kupitia kuta za mishipa ya damu iliyoharibika kwenye fizi. Vikishaingia kwenye mzunguko wa damu, vinaweza kusafiri hadi kufikia mishipa ya damu ndani ya ubongo.
Kwa mfano, uvimbe unaotokana na magonjwa ya fizi (kama vile 'periodontitis' au ugonjwa wa kuoza kwa fizi) au hata bakteria wenyewe kutoka mdomoni, vinaweza kusababisha au kuzidisha uvimbe kwenye mishipa ya damu ya ubongo. Hali hii inaweza kuongeza hatari ya kupata magonjwa hatari kama kiharusi (stroke), kupungua kwa uwezo wa kufikiri na kukumbuka (cognitive decline), na hata ugonjwa wa kusahau wa Alzheimer's. Swali linalojitokeza ni je, inawezekana kutumia aina ya bakteria waliopo mdomoni kama kiashiria cha kutabiri hatari ya kupata ugonjwa wa sahau?
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Exeter nchini Uingereza walifanya uchunguzi kwa watu wazima 115 wenye umri wa miaka 50 na zaidi. Walichunguza mate yao ili kubaini aina za bakteria wa mdomoni ambao wanaweza kuwa na uhusiano na afya ya ubongo, hasa uwezo wa utambuzi. Kati ya washiriki, asilimia 52 walikuwa na uwezo mzuri wa kiakili, wakati asilimia 48 walikuwa na dalili za upungufu mdogo wa utambuzi (Mild Cognitive Impairment - MCI), ikiwemo kusahau. Matokeo ya utafiti huu yalichapishwa katika jarida la kisayansi la kimataifa 'PNAS Nexus'.
Uchambuzi wa mate ya washiriki ulibaini kuwa makundi mawili ya bakteria, Neisseria na Haemophilus, yalihusishwa na afya bora ya ubongo. Watu waliokuwa na viwango vya juu vya bakteria hawa walifanya vizuri zaidi katika vipimo vya uwezo wa kiakili, hasa kwenye maeneo ya kumbukumbu, umakini, na uwezo wa kufanya kazi ngumu zinazohitaji kufikiri kwa kina. Zaidi ya hayo, mate ya watu hawa yalikutwa na viwango vya juu vya kemikali iitwayo 'nitrite'. Nitrite huzalishwa wakati bakteria wanapovunja vunja kemikali nyingine iitwayo 'nitrate' inayopatikana kwa wingi kwenye mboga za majani kama vile mchicha.
Bakteria hawa wa mdomoni husaidia kuzalisha 'nitric oxide' kutokana na kuvunja vunja 'nitrite'. Nitric oxide inajulikana kwa kusaidia kutanua mishipa ya damu, hivyo kuboresha mzunguko wa damu na kupunguza shinikizo la damu. Watafiti wanasema hii inaashiria kuwa ulaji wa mboga zenye nitrate kwa wingi, kama mchicha, unaweza kusaidia kuongeza idadi ya bakteria hawa wazuri na hivyo kuchangia katika afya bora ya ubongo.
Watafiti hao waliongeza kuwa wanaendelea na utafiti mwingine kuangalia kama unywaji wa juisi ya beetroot (ambayo pia ina nitrate nyingi) unaweza kuboresha utendaji kazi wa ubongo kupitia ushawishi wake kwa bakteria wa mdomoni.
Hata hivyo, utafiti huo pia uligundua aina nyingine za bakteria wa mdomoni ambazo zinaonekana kuwa na athari hasi kwa afya ya ubongo. Watu walioonyesha matatizo ya kumbukumbu walikutwa na viwango vya juu vya bakteria aina ya Porphyromonas, ambao kwa kawaida huhusishwa na magonjwa ya fizi.
Aidha, bakteria wengine waitwao Prevotella walionekana kuhusishwa na kupungua kwa uwezo wa kiakili. Bakteria hawa walikuwa wengi zaidi kwa watu waliokuwa na viwango vya chini vya 'nitrite' kwenye mate yao. Pia, ilionekana kuwa watu wenye vinasaba (jeni) vinavyoongeza hatari ya kupata Alzheimer's (APOE4) walikuwa na viwango vya juu zaidi vya Prevotella. Hata hivyo, watafiti wanasisitiza kuwa huu ni uhusiano wa kuambatana tu, na bado hawajathibitisha kama Prevotella ndio chanzo cha moja kwa moja cha kupungua kwa uwezo wa kiakili.
Matokeo ya utafiti huu yanaunga mkono tafiti nyingine za hivi karibuni zinazoonyesha uhusiano kati ya afya ya kinywa na ugonjwa wa sahau. Kwa mfano, utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Tohoku nchini Japan ulionyesha uhusiano kati ya ugonjwa wa fizi na kupungua kwa ukubwa wa sehemu ya ubongo iitwayo 'hippocampus', ambayo ni muhimu kwa kumbukumbu. Utafiti mwingine kutoka Chuo Kikuu cha Louisville nchini Marekani uligundua bakteria wa Porphyromonas (wanaosababisha ugonjwa wa fizi) kwenye ubongo wa watu waliokufa wakiwa na ugonjwa wa Alzheimer's. Majaribio kwa panya yalionyesha kuwa panya walioambukizwa bakteria hawa walizalisha kwa wingi protini ya 'amyloid-beta', ambayo ni kiashiria kikuu cha Alzheimer's kwenye ubongo.
Watafiti wanaamini kuwa matokeo haya ni muhimu sana. Ikiwa itathibitika kuwa kuna bakteria mahususi wanaosaidia kulinda ubongo na wengine wanaodhuru, basi mbinu za kimatibabu zinazolenga kubadilisha uwiano wa bakteria mdomoni zinaweza kuwa sehemu ya mikakati ya kuzuia ugonjwa wa sahau siku zijazo. Kwa mfano, kuhamasisha ukuaji wa bakteria wazalishaji wa 'nitrite' kama Neisseria na kupunguza idadi ya Prevotella na Porphyromonas kunaweza kusaidia kupunguza kasi ya kudhoofika kwa ubongo kunakoletwa na kuzeeka.
Pia, wanapendekeza kuwa huenda siku za usoni vipimo vya kupima viwango vya bakteria hawa vikawa sehemu ya ukaguzi wa kawaida wa meno, ili kusaidia kugundua dalili za mapema za hatari ya kudhoofika kwa afya ya ubongo.
Dkt. Joanna Lehr, mtafiti aliyeongoza utafiti huu, aliandika kwenye makala kwa 'The Conversation' akisema, "Iwapo itathibitika kuwa jamii ya viumbe hai vidogo mdomoni (oral microbiome) ina jukumu muhimu katika afya ya ubongo, basi kunaweza kufunguka njia mpya za kugundua mapema na kuchelewesha ugonjwa wa sahau kupitia udhibiti wa bakteria wa mdomoni." Alihitimisha, "Hadi wakati huo utakapofika, njia bora zaidi ni kutunza meno yako vizuri kwa usafi na kula vyakula vyenye nitrate nyingi kama mboga za majani ili kuongeza bakteria wazuri mdomoni mwako."