Watu ambao hawalali vizuri wana uwezekano mkubwa wa kuwa na 'ubongo uliozeeka' kuliko wale wanaopata usingizi wa kutosha. Utafiti mpya umethibitisha uhusiano mkubwa kati ya ukosefu wa usingizi na kuzeeka kwa haraka kwa ubongo.
Timu ya watafiti ikiongozwa na Abigail Dove kutoka Taasisi ya Karolinska nchini Uswidi, ilichapisha matokeo yao katika jarida la kimataifa la eBioMedicine.
Watafiti walichambua data za kliniki kutoka Benki ya Bio ya Uingereza, zikijumuisha picha za skana ya ubongo (MRI) za watu wazima na wazee 27,500. Walitumia mfumo wa machine learning uliofundishwa na sifa za ubongo zinazoonekana kwenye MRI, ili kukadiria umri wa kibiolojia wa ubongo wa kila mshiriki.
Watafiti walipima ubora wa usingizi wa washiriki kwa kutumia mfumo wa kujiripoti wa mambo matano:
- Chronotype (Kama mtu anapenda kulala mapema au kuchelewa).
- Muda wa Kulala.
- Tatizo la Kukosa Usingizi (Insomnia).
- Kukoroma.
- Kusinziasinzia wakati wa mchana.
Kulingana na alama za ubora wa usingizi walizopata, washiriki waligawanywa katika makundi matatu: Kikundi chenye Afya (alama 4 au zaidi), Kikundi cha Wastani (alama 2-3), na Kikundi chenye Upungufu wa Usingizi (alama 1 au chini).
Uchambuzi ulionyesha uhusiano wa wazi: Kila alama moja ya ubora wa usingizi iliyopungua, kulikuwa na tofauti ya miezi sita kati ya umri wa kibiolojia wa ubongo na umri halisi wa mtu. Hii inamaanisha kwamba mtu mwenye ubora mbaya wa usingizi anakuwa na ubongo unaoonekana kuwa mkubwa zaidi kuliko umri wake halisi.
Sababu za Muunganisho Huu
Watafiti waligundua kuwa zaidi ya asilimia 10 ya uhusiano kati ya usingizi mbaya na kuzeeka kwa ubongo unaweza kuelezewa na kiwango cha uvimbe (inflammation) mwilini.
"Upungufu wa usingizi unachangia kuongezeka kwa uvimbe, na uvimbe huu ni mojawapo ya sababu kuu za kuzeeka kwa ubongo," watafiti walieleza. Wanaeleza kuwa kwa kuwa muda wa kulala na viwango vya uvimbe mwilini vinaweza kudhibitiwa, watu wanaweza kuzuia kuzeeka kwa haraka kwa ubongo na kupungua kwa utendaji wa akili (cognitive decline) kwa kuishi maisha yenye afya.
Sababu nyingine inayoelezea uhusiano huu ni jukumu la ubongo wakati wa kulala. Wakati mtu anapokuwa usingizini, ubongo huendesha mfumo wa kuondoa taka na sumu. Ukosefu wa usingizi hufanya taka hizo zisitolewe vizuri, na hivyo kuathiri afya ya ubongo.
Pia, ukosefu wa usingizi huathiri vibaya mfumo wa moyo na mishipa ya damu, jambo ambalo linaweza kuongeza kasi ya kuzeeka kwa ubongo.