Rais wa Marekani, Donald Trump, amesaini amri ya utendaji yenye lengo la kufunga Wizara ya Elimu ya Marekani, hatua ambayo imezua mjadala mkubwa nchini humo. Trump, ambaye alitoa tangazo hilo tarehe 20 Machi, amesisitiza kuwa serikali yake itatumia kila njia ya kisheria kuhakikisha kuwa wizara hiyo inafungwa rasmi. Hata hivyo, mpango huo unakabiliwa na kikwazo kikubwa katika Bunge la Marekani, hasa katika Seneti, ambako unahitaji kupata kura 60 ili kupitishwa, wakati chama chake cha Republican kina viti 53 pekee.
Katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House, Trump alieleza kuwa lengo lake ni kurudisha mamlaka ya kusimamia elimu kwa serikali za majimbo. Alidai kuwa magavana wengi wana uwezo mkubwa wa kuboresha elimu katika maeneo yao kuliko serikali kuu. "Tunataka kuwarudisha wanafunzi kwa majimbo yao. Kuna magavana ambao wana shauku kubwa ya kurudishiwa mamlaka ya elimu na wanaweza kufanya kazi nzuri," alisema Trump.
Trump alikosoa vikali Wizara ya Elimu, akidai kuwa imekuwa ikisimamiwa na wapinzani wa kihafidhina na imeshindwa kuleta matokeo chanya. Alitaja kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa Marekani katika masomo ya kusoma, hesabu na sayansi kama ushahidi wa kutotosheleza kwa wizara hiyo. Aliongeza kuwa mfumo mpya bila wizara hiyo utawezesha shule za Marekani kushindana na shule za Ulaya na China.
Pamoja na amri hiyo, Trump alitoa tamko la kibinafsi la kuwapongeza walimu na kuwatambua kama watu muhimu sana kwa taifa. Aliwataka vyama vya wafanyakazi wa walimu kushirikiana naye. "Iwe wako kwenye chama au la, tutawahudumia walimu," alisema.
Wakati akisaini amri hiyo, Trump alikuwa ameandamana na wanafunzi wa rika mbalimbali, ambao walikuwa wameketi kwenye madawati kama shuleni, wakionyesha maandiko ya amri hiyo. Pia, alimwambia Waziri wa Elimu, Linda McMahon, kuwa hatarajii akae muda mrefu katika nafasi hiyo, akiongeza, "Tutakutafutia kazi nyingine."
Mpango wa Trump kufunga Wizara ya Elimu si mpya na umekuwa ukizungumziwa tangu kampeni zake za awali. Kimsingi, elimu nchini Marekani imekuwa ikisimamiwa na serikali za majimbo na mamlaka za mitaa, huku serikali kuu ikitoa asilimia 8-10 tu ya bajeti ya elimu.
Hata hivyo, wizara hiyo ina jukumu muhimu katika kusimamia mipango ya misaada kama ule wa Title 1, ambao unagharimu dola bilioni 18.4 (takriban TZS trilioni 47.2) kwa shule zenye wanafunzi kutoka familia masikini, na dola bilioni 15.5 (takriban TZS trilioni 39.8) kwa elimu ya watoto wenye ulemavu. Pia, inasimamia mikopo ya elimu ya juu yenye thamani ya dola trilioni 1.6 (takriban TZS trilioni 4,104), pamoja na ruzuku za serikali kwa wanafunzi wa vyuo.
Trump amesema kuwa hatakusudia kufuta huduma hizo muhimu, bali atazihamishia kwenye taasisi nyingine za serikali. "Tutahifadhi rasilimali hizo na kuzisambaza kwa taasisi tofauti zitakazozisimamia vizuri," alisema.
Hata hivyo, utekelezaji wa kufungwa kwa wizara hiyo bado unakabiliwa na changamoto kubwa. Waziri McMahon alikubali kuwa ni Bunge la Marekani pekee lenye uwezo wa kuifuta Wizara ya Elimu, kwani ndilo lililoianzisha mwaka 1979. Alipendekeza baadhi ya kazi za wizara hiyo zihamishiwe kwenye taasisi nyingine, lakini wataalamu wameonya kuwa hata hivyo, uidhinishaji wa bunge unahitajika.
Kulingana na ripoti ya CNN, serikali ya Trump inakabiliwa na ugumu wa kutafuta taasisi mbadala itakayoweza kusimamia mpango wa mikopo ya wanafunzi, ambao deni lake limefikia dola trilioni 1.8 (takriban TZS trilioni 4,617), huku asilimia 40 ya mikopo hiyo ikiwa imechelewa kulipwa.
Trump tayari ameanza kupunguza wafanyakazi wa Wizara ya Elimu kwa karibu nusu na kufuta mikataba na ruzuku kadhaa, jambo linaloonyesha azma yake ya kulifanikisha pendekezo hilo, licha ya vikwazo vya kisheria na kisiasa vinavyoendelea kuibuka.