Serikali ya Rwanda imethibitisha kupokea kundi la kwanza la wahamiaji saba waliofurushwa kutoka nchini Marekani, ikiwa ni sehemu ya makubaliano mapya yenye utata kati ya nchi hizo mbili. Tukio hili linaashiria utekelezaji wa sera ya Utawala wa Rais Donald Trump ya kuwapeleka wahamiaji haramu katika "nchi ya tatu" iwapo nchi zao za asili zitakataa kuwapokea.
Msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo, alitoa taarifa akisema kuwa kundi hilo la kwanza la wahamiaji liliwasili nchini humo katikati ya mwezi Agosti. Baada ya kuhojiwa, wahamiaji watatu walieleza nia yao ya kurejea katika nchi zao za asili, huku wanne waliosalia wakiomba kubaki na kuendelea na maisha nchini Rwanda. Hata hivyo, mataifa ya asili ya wahamiaji hao saba hayakuwekwa wazi.
Bi. Makolo aliongeza kuwa wahamiaji hao wamehifadhiwa katika vituo maalum chini ya usimamizi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na mashirika ya huduma za jamii nchini Rwanda. Kuwasili kwao kunafuatia makubaliano yaliyofikiwa mapema mwezi huu, ambapo Rwanda ilikubali kupokea hadi wahamiaji 250 watakaoondolewa nchini Marekani.
Sera hii ni matokeo ya msimamo mkali wa Rais Trump dhidi ya wahamiaji wasio na vibali, ambapo alianzisha mpango wa kuwasaka na kuwarejesha makwao. Chini ya mpango huo, Marekani ilitafuta ushirikiano na nchi nyingine ili ziweze kuwapokea wahamiaji ambao nchi zao zinagoma kuwachukua.
Katika bara la Afrika, mataifa manne yameingia katika makubaliano hayo na Marekani; Rwanda, Uganda, Sudan Kusini, na Eswatini. Hii si mara ya kwanza kwa Marekani kutekeleleza sera hii. Mwezi Mei, wahamiaji 10 kutoka nchi kama Vietnam, Laos, Thailand na Pakistan walifurushwa na kupelekwa nchini Sudan Kusini. Mwezi uliopita, wahamiaji wengine watano walipelekwa Eswatini. Inafahamika kuwa hakuna hata mmoja kati ya wahamiaji hao aliyekuwa raia wa Sudan Kusini au Eswatini.
Sera hii imekosolewa vikali na wanaharakati wa haki za binadamu, ambao wanaonya kuwa inawaweka wahamiaji katika hatari ya kupelekwa kwenye nchi ambazo wanaweza kukumbana na madhara au mateso, na ambazo hawana uhusiano nazo kabisa.