Marekani Yaendelea 'Kutupa' Wahamiaji Afrika, Sasa ni Zamu ya Ghana

international | Fri Sep 12 2025


Marekani Yaendelea 'Kutupa' Wahamiaji Afrika, Sasa ni Zamu ya Ghana

Ghana imejiunga rasmi na orodha inayoongezeka ya nchi za Kiafrika zilizokubali kuwapokea wahamiaji wanaofukuzwa kutoka Marekani, hata kama sio raia wake. Rais wa Ghana, John Mahama, alithibitisha juzi usiku kuwa nchi yake imeshawapokea wahamiaji 14 waliofukuzwa, wote wakiwa raia wa nchi mbalimbali za Afrika Magharibi.


Kwa hatua hii, Ghana inakuwa nchi ya nne barani Afrika kukubali mpango huu wenye utata, ikiungana na Uganda, Rwanda, na Sudan Kusini. Hata hivyo, ni nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Magharibi kuingia makubaliano ya aina hii na Marekani.


Akitetea uamuzi huo, Rais Mahama alisema serikali yake ilikubaliana na Marekani kwa sababu sheria za Ghana hazimlazimishi raia yeyote kutoka nchi ya Afrika Magharibi kuwa na viza ili kuingia nchini humo, kwa mujibu wa itifaki za Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS).


"Tulikubaliana na Marekani kuwapokea kwa sababu raia wote wa Afrika Magharibi hawaitaji viza kuja Ghana," alisema Rais Mahama.


Alithibitisha kuwa wahamiaji hao 14 tayari wamewasili nchini humo na kueleza kuwa wale wenye asili ya Nigeria na Gambia watarejeshwa kwenye nchi zao. Hata hivyo, Rais Mahama hakueleza iwapo wahamiaji hao walikuwa na rekodi za uhalifu, suala ambalo limekuwa likizua wasiwasi mkubwa katika mikataba kama hii.


Sera hii ya kuwafukuza wahamiaji na kuwapeleka nchi ya tatu ni sehemu ya msako mkali unaoendeshwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, katika muhula wake wa pili, unaowalenga wahamiaji walio na rekodi za uhalifu na wale waliozidi muda wao wa kuishi nchini humo. Uamuzi wa Ghana unafungua ukurasa mpya katika siasa za uhamiaji kati ya Marekani na ukanda wa Afrika Magharibi.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.