"Nilihisi kama nilikuwa natekwa nyara wakati Marekani iliponipeleka Sudan Kusini," haya ni maneno ya Jesús Muñoz-Gutiérrez, raia wa Mexico, alipowasili uwanja wa ndege wa Juba. Kisa chake kimeanika sera mpya ya kutisha na yenye utata ya serikali ya Rais Donald Trump, ya kuwafukuza wahamiaji wasio na vibali na kuwapeleka katika nchi za Afrika ambazo hawana uhusiano nazo hata kidogo.
Chini ya sera hii, serikali ya Marekani imeingia makubaliano na baadhi ya nchi za Afrika kukubali kupokea wahamiaji wanaofukuzwa kutoka Marekani, hata kama sio raia wa nchi hizo. Hadi sasa, nchi tano—Sudan Kusini, Eswatini, Rwanda, Uganda, na Ghana—zimeripotiwa kukubali mpango huu.
Muñoz-Gutiérrez alikuwa mmoja wa watu wanane waliofukuzwa kutoka Marekani na kupelekwa Sudan Kusini mwezi Julai, nchi yenye vita vya wenyewe kwa wenyewe na hali mbaya ya usalama. Licha ya nchi yake ya Mexico kuwa tayari kumpokea, Marekani iliamua kumpeleka Sudan Kusini, kitendo kinachokiuka vikali sheria za kimataifa na haki za binadamu.
Sera hii imegeuza baadhi ya nchi za Afrika kuwa maeneo ya "kutupia" watu ambao Marekani haiwataki. Mwezi Julai, Eswatini ilipokea watu watano kutoka Vietnam, Jamaica, Cuba, Yemen na Laos, wote wakiwa na rekodi za uhalifu. Rwanda ilipokea watu saba mwezi Agosti, na Ghana imethibitisha kupokea watu 14 kutoka nchi mbalimbali za Afrika Magharibi.
Hali hii imezua ghadhabu kubwa barani Afrika. Shirika la haki za binadamu nchini Eswatini lilisema, "Hatuwezi kuwa jaa la taka la Marekani." Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria ameonya Marekani dhidi ya kutumia mbinu za kuwekea vikwazo vya viza kuzishinikiza nchi za Afrika kukubali mipango hiyo. Vyama vya upinzani nchini Rwanda na Sudan Kusini vimezishutumu serikali zao kwa kusalimu amri kwa shinikizo la Marekani na kuhatarisha haki za binadamu.
Wachambuzi wanasema hii ni biashara ya kisiasa inayokiuka misingi ya utawala wa sheria, ambapo Marekani, yenye rasilimali na mifumo imara, inakwepa jukumu lake na kuutupa mzigo kwa mataifa dhaifu ya Kiafrika. Licha ya upinzani, Rais Trump anaendelea kushinikiza nchi nyingine za Afrika, ikiwemo Gabon, Liberia na Senegal, kukubali mpango huo.
Kisa cha Muñoz-Gutiérrez, ambaye sasa amerejeshwa Mexico baada ya kuishi kizuizini Sudan Kusini, kinaonesha ukatili wa sera hii. Kuna wito sasa kwa Umoja wa Afrika (AU) na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuingilia kati na kupinga vikali mwenendo huu, ambao unahatarisha mfumo mzima wa haki za binadamu duniani na kugeuza watu walio katika mazingira magumu kuwa bidhaa za kisiasa.