Hali ya wasiwasi imeibuka upya katika Bahari ya Kusini ya China baada ya serikali ya Beijing kutangaza kuanzisha hifadhi ya taifa ya mazingira katika eneo la Tumbawe la Scarborough, ambalo limekuwa chanzo cha mzozo wa muda mrefu wa umiliki kati yake na Ufilipino. Hatua hii, ambayo inatafsiriwa kama njama ya China ya kuimarisha udhibiti wake kwenye eneo hilo lenye utajiri wa maliasili, imezua hasira kali kutoka kwa serikali ya Ufilipino.
Mnamo tarehe 10 mwezi huu, Baraza la Serikali la China liliidhinisha pendekezo la Wizara ya Maliasili la kugeuza eneo hilo, linalojulikana kama Huangyan Dao kwa Kichina, kuwa hifadhi ya asili. Kwa mujibu wa taarifa rasmi, lengo kuu ni "kulinda mfumo wa ikolojia." Hifadhi hiyo mpya inakadiriwa kuwa na ukubwa wa hekta 3,523.67, ambapo sehemu kubwa imetengwa kama eneo la msingi linalohitaji ulinzi mkali.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanaona hatua hii kama mkakati wa kisiasa. Mtafiti kutoka Taasisi ya Mikakati ya Maendeleo ya Bahari ya China, Luo Gang, aliliambia gazeti la Global Times kwamba kanuni za hifadhi za asili zitafuata kwa ukamilifu. Alisisitiza kuwa shughuli zote za kibinadamu kama vile uvuvi, ukataji miti, uwindaji, uchimbaji madini, na hata ukusanyaji wa mitishamba zitapigwa marufuku kabisa ndani ya mipaka ya hifadhi.
Luo alifafanua zaidi kuwa kuingia katika eneo la msingi la hifadhi kutaruhusiwa tu kwa shughuli za kisayansi zilizoidhinishwa na serikali ya China. "Mtu yeyote au taasisi, hasa wageni kutoka nchi za nje, watahitajika kupata kibali maalum kutoka kwa mamlaka za China kabla ya kuingia. Yeyote atakayekiuka sheria hizi kwa kuingia bila ruhusa au kufanya shughuli haramu, atachukuliwa hatua kali za kisheria," alionya Luo, kauli inayoonekana kulenga moja kwa moja Ufilipino.
Serikali ya Ufilipino haikuchelewa kujibu, ambapo siku moja baada ya tangazo hilo, ilitoa taarifa kali ikieleza kuwa hatua ya China ni "haramu" na inakiuka waziwazi haki na maslahi ya taifa lao. Ufilipino imeitaka China kuachana na mpango huo na kuheshimu sheria za kimataifa, ikiwemo Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria za Bahari wa mwaka 1982.
Mvutano huu unaongezwa nguvu na harakati za kijeshi za China katika ukanda huo. Hivi karibuni, meli yake mpya ya tatu ya kubeba ndege za kivita, iitwayo Fujian, imeonekana ikifanya majaribio na mazoezi katika Bahari ya Kusini ya China na kupita katika Mlango wa Bahari wa Taiwan. Ingawa msemaji wa Jeshi la Wanamaji la China amesema mazoezi hayo hayalengi taifa lolote, wachambuzi wanaona kama onyesho la nguvu linaloendana na hatua za kisiasa kama hii ya kuanzisha hifadhi. Hata wizara ya ulinzi ya Japani imethibitisha kuiona meli hiyo ya Fujian ikisafiri kusini mwa Bahari ya Mashariki ya China, ikisindikizwa na meli nyingine mbili za kivita.