Wakati dunia inashuhudia msukumo mkubwa wa teknolojia ya akili mnemba (AI), inayochochewa na mifumo kama ChatGPT ya Marekani na DeepSeek ya China, taswira ya giza inaanza kujitokeza kuhusu mustakabali wa ajira. Hofu inazidi kuongezeka kuwa kadri matumizi ya AI yanavyosambaa, ndivyo idadi ya nafasi za kazi itakavyopungua, hasa katika sekta za utafutaji taarifa na huduma kwa wateja, na hivyo kusababisha ukosefu wa ajira na kuyumbisha soko la ajira.
Dalili za wazi za mwelekeo huu zimeonekana hivi karibuni. Kituo cha habari za kiuchumi cha CNBC nchini Marekani kimeripoti kuwa Marc Benioff, Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni kubwa ya huduma kwa wateja ya Salesforce, amethibitisha kupunguza ajira 4,000 katika idara ya usaidizi kwa wateja pekee.
Akizungumza kwenye kipindi cha podcast cha 'The Logan Bartlett Show', Benioff alifafanua jinsi AI imeathiri uendeshaji wa kampuni yake, akisema mahitaji ya wafanyakazi yamepungua kwa kiasi kikubwa. "Tumepunguza idadi kutoka wafanyakazi 9,000 hadi takriban 5,000," alisema, akionyesha ukubwa wa mabadiliko hayo.
Awali, Benioff alikuwa ameweka wazi kuwa AI tayari inafanya kati ya asilimia 30 hadi 50 ya kazi zote ndani ya Salesforce. Alisema, "Sasa sote tunapaswa kukubaliana na uhalisia kwamba AI itafanya kazi zilizokuwa zikifanywa na binadamu, na sisi tutahamia kwenye shughuli zenye tija ya juu zaidi." Kauli hii inathibitishwa na hatua ya kampuni hiyo kubuni mfumo wa AI ujulikanao kama 'Agentforce', ambao umeongeza ufanisi na kuondoa hitaji la kuajiri wahandisi wa usaidizi kwa wateja.
Kampuni nyingine kubwa, Microsoft, pia imechukua hatua kama hiyo. Mwaka huu, kampuni hiyo ilipanga upya biashara zake kuipa kipaumbele AI na katika nusu ya kwanza ya mwaka pekee, ilipunguza wafanyakazi 15,000, hasa katika idara za mauzo na utengenezaji wa programu. Hili ni punguzo kubwa zaidi tangu walipoachisha kazi watu 10,000 mwaka 2023.
Wataalamu wanaonya kuwa uwezo wa AI kushughulikia kazi rahisi na hata zile ngumu zinazohitaji uchambuzi wa taarifa utazidisha tatizo la upotevu wa ajira. Mshauri wa rasilimali watu, Lori Ruettimann, anasema, "Kote nchini Marekani, watu wanaachishwa kazi kwa sababu ya moja kwa moja ya AI," na kusisitiza kuwa yeyote anayetaka kubaki kazini au kupata kazi mpya lazima ajifunze stadi mpya za kiteknolojia.
Utabiri wa kutisha zaidi umetolewa na Dario Amodei, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya AI ya Anthropic, aliyesema, "AI inaweza kuchukua nafasi ya nusu ya ajira zote za maofisini za ngazi ya chini. Ndani ya mwaka mmoja hadi mitano, kiwango cha ukosefu wa ajira kinaweza kufikia asilimia 20."