Urusi imefanya shambulio kubwa zaidi la anga dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, katika kipindi cha mwezi mmoja, na hivyo kuzorotesha matumaini ya mazungumzo ya amani yaliyokuwa yanaanza kupata msukumo. Mashambulizi hayo ya kinyama hayakuacha hata ofisi za kidiplomasia, ambapo majengo ya Umoja wa Ulaya (EU) na Ubalozi wa Uingereza yalipata uharibifu.
Kwa mujibu wa taarifa za kimataifa, shambulio hilo la usiku wa manane lilisababisha vifo vya watu 15, wakiwemo watoto wane, huku wengine 38 wakijeruhiwa. Vikosi vya uokoaji vinaendelea na kazi ya kuwatafuta watu walionaswa kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka. Jeshi la Anga la Ukraine limesema kuwa Urusi ilirusha jumla ya droni 598, makombora ya masafa marefu 11, na makombora ya cruise 20 kote nchini, ingawa walidai kufanikiwa kuzuia mengi yao.
Shambulio hili linakuja wakati ambapo juhudi za kidiplomasia za kusaka amani, zikiongozwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, zilikuwa zimeanza kuzaa matunda. Trump alikuwa amefanya mkutano na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, na alikuwa katika mchakato wa kujadili na viongozi wa Ukraine na Ulaya kuhusu mipango ya usalama baada ya vita.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, alionesha kukerwa kwake vikali, akisema Urusi imejibu wito wa dunia wa kusitisha mapigano kwa kutumia makombora badala ya kukaa kwenye meza ya mazungumzo. "Huu ni ujumbe wa Urusi kwa wale wote duniani ambao wamekuwa wakihimiza diplomasia ya kweli kwa wiki na miezi kadhaa. Badala ya meza ya mazungumzo, Urusi imechagua silaha za maangamizi," Zelenskyy alisema kupitia mtandao wa X, akitaka vikwazo vipya na vikali zaidi dhidi ya Urusi.
Viongozi wa Ulaya nao wamelaani vikali shambulio hilo. Rais wa Halmashauri Kuu ya EU, Ursula von der Leyen, alieleza hasira yake kwa kushambuliwa kwa ofisi za EU, akisema: "Baada ya kuwatia hofu raia na kuua watu bila kujali umri wala jinsia, sasa Urusi inalenga hadi Umoja wa Ulaya." Alitangaza mara moja kuanza kwa mchakato wa kuiwekea Urusi vikwazo zaidi na kutumia mali zake zilizozuiliwa kwa ajili ya kuijenga upya Ukraine.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, pia walitoa kauli kali, wakilitaja shambulio hilo kuwa ni kitendo cha ugaidi na unyama kinacholenga kuharibu matumaini yote ya amani.
Kwa upande wake, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imedai kuwa mashambulizi yake yalilenga vituo vya kijeshi na viwanja vya ndege vya Ukraine, na kwamba haikulenga raia kimakusudi. Ikulu ya Kremlin pia ilisisitiza kuwa bado ina nia ya kufanya mazungumzo, licha ya kuendeleza mashambulizi dhidi ya jeshi la Ukraine.