Kivumbi kimetimka tena nchini Marekani kufuatia Chama cha Democratic kufichua nyaraka mpya zinazomhusisha aliyekuwa bilionea na mwekezaji wa Wall Street, Jeffrey Epstein, na majina ya watu mashuhuri duniani, wakiwemo Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Tesla, Elon Musk. Epstein, ambaye alikutwa amejinyonga gerezani akisubiri kesi ya ulawiti na usafirishaji haramu wa wasichana wadogo, ameacha historia iliyojaa utata na maswali mengi yasiyo na majibu.
Nyaraka hizi za sasa, zilizotolewa hivi karibuni, zimeweka wazi kuwa Elon Musk alialikwa kwenye kisiwa cha faragha cha Epstein mnamo Desemba 6, 2014. Hata hivyo, punde tu baada ya taarifa hizi kuenea, Musk alitumia mtandao wake wa kijamii wa X (zamani Twitter) kukanusha vikali, akiziita tuhuma hizo kuwa ni "uongo mtupu." Kitendo hiki kimezua mjadala mkubwa mtandaoni kuhusu ukweli wa madai hayo.
Mbali na Musk, jina la Mwanamfalme Andrew wa Uingereza, ambaye ni mdogo wake Mfalme Charles III, limeonekana tena kwenye orodha hiyo. Nyaraka zinaonyesha kuwa mwezi Mei mwaka 2000, Mwanamfalme Andrew alisafiri kwa ndege kutoka New Jersey kuelekea Florida akiwa pamoja na Epstein na kundi lake. Ingawa hii si mara ya kwanza kwa Mwanamfalme Andrew kuhusishwa na kashfa hii, amekuwa akikanusha mara kwa mara kuhusika kwake katika vitendo vyovyote vya kihalifu vinavyomuhusu Epstein.
Jeffrey Epstein alijijengea sifa ya kuwa na urafiki na watu wenye nguvu na ushawishi mkubwa duniani, kuanzia wanasiasa kama aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump, hadi wafanyabiashara wakubwa na wasomi. Nguvu yake ya kifedha na mtandao mpana viliaminika kumlinda kwa muda mrefu.
Historia ya uhalifu ya Epstein ilianza kuwekwa wazi mwaka 2006 alipokamatwa kwa makosa ya kufanya ngono na kulawiti wasichana takriban 30 walio chini ya umri. Licha ya uzito wa makosa hayo, alihukumiwa kifungo chepesi cha miezi 18 na akapewa upendeleo wa kuwa "mfungwa wa mfano," uliomruhusu kutoka nje ya gereza wakati wa mchana na kurudi usiku. Hali ilizidi kuwa ya kushangaza alipoachiliwa miezi mitatu kabla ya muda wake, na kufanya atumikie kifungo cha miezi 15 pekee.
Mnamo Julai 2019, Epstein alikamatwa tena na polisi wa New York kwa kushirikiana na Shirika la Upelelezi la FBI, akikabiliwa na tuhuma mpya za makosa ya kingono dhidi ya wasichana wengine zaidi ya 20 kati ya mwaka 2002 na 2005. Mwezi mmoja tu baada ya kukamatwa, Epstein alikutwa amefariki katika chumba chake cha gereza huko Manhattan, kifo ambacho kilielezwa rasmi kuwa ni cha kujinyonga, ingawa kimeacha nadharia nyingi za njama zikiendelea kuzagaa hadi leo.