Kimbunga Marekani: Siri za 'Bosi' Epstein Kuanikwa Hadharani, Vigogo wa Dunia Roho Mkononi

international | Thu Dec 11 2025


Kimbunga Marekani: Siri za 'Bosi' Epstein Kuanikwa Hadharani, Vigogo wa Dunia Roho Mkononi

Hali ya taharuki na tumbo joto imewakumba vigogo, wanasiasa, na matajiri wakubwa duniani baada ya Mahakama ya Shirikisho nchini Marekani kuamuru kufunguliwa kwa "sanduku la Pandora" linalohusu skandali nzito ya ngono ya marehemu bilionea Jeffrey Epstein. Uamuzi huu umekuja kama radi isiyotarajiwa, ukilenga kuweka hadharani nyaraka za siri zilizokuwa zimefichwa kwa muda mrefu kuhusu biashara haramu ya ngono iliyohusisha wasichana wadogo na baadhi ya watu wenye nguvu zaidi duniani.


Jaji Richard Berman wa Mahakama ya Wilaya ya Kusini mwa New York, amekubali ombi la Wizara ya Sheria ya Marekani la kutaka kuwekwa wazi kwa nyaraka za Baraza la Mahakama (Grand Jury) zinazohusiana na mashtaka ya Epstein. Hatua hii ni utekelezaji wa sheria mpya iliyopitishwa na Bunge la Marekani mwezi uliopita, inayojulikana kama "Epstein Files Transparency Act" (Sheria ya Uwazi ya Mafaili ya Epstein), ambayo inalenga kuzuia kufunikwa kwa kombe ili mwanaharamu apite katika sakata hili linaloumiza vichwa wengi.


Kulingana na sheria hiyo mpya, Mwanasheria Mkuu wa Marekani amepewa makataa hadi Desemba 19, mwaka huu, kuhakikisha kuwa nyaraka zote za siri, mawasiliano, na ripoti za uchunguzi zinazomuhusu Epstein na mpambe wake wa karibu, Ghislaine Maxwell, zinatolewa kwa umma. Hii inamaanisha kuwa kuanzia wiki ijayo, dunia inaweza kushuhudia majina mazito yakitajwa katika kashfa hii, jambo linaloweza kubadili upepo wa kisiasa na kijamii nchini Marekani na kwingineko.


Siku moja kabla ya uamuzi wa Jaji Berman, Jaji mwingine wa mahakama hiyo, Paul Engelmayer, naye aligonga nyundo kuamuru kutolewa kwa ushahidi uliotolewa na Ghislaine Maxwell, ambaye alikuwa mpenzi na mshirika mkuu wa Epstein katika kusuka mtandao huo wa unyanyasaji wa kingono. Maxwell kwa sasa anatumikia kifungo jela kwa makosa ya kuwatafutia wasichana wadogo Epstein ili awatumie kingono.


Jeffrey Epstein, ambaye alikuwa meneja wa fedha za ua (Hedge Fund Manager) na bilionea mwenye ushawishi mkubwa, alikamatwa mwaka 2019 kwa tuhuma za kuendesha biashara ya ngono iliyowahusisha wasichana wadogo (minors) katika makazi yake ya kifahari jijini New York, Florida, na katika kisiwa chake binafsi kilichopo Virgin Islands. Hata hivyo, alikutwa amekufa katika selo yake gerezani mwezi Agosti 2019, kifo ambacho mamlaka zilisema ni kujinyonga, ingawa wengi wanaamini kuna mkono wa mtu au "Deep State" ili kuziba mdomo wake usitaje majina ya washirika wake.


Katika kile kinachoonekana kama kulinda utu, Jaji Berman ametoa angalizo kali kuwa wakati nyaraka hizo zikitolewa, lazima utambulisho na faragha za wahanga (victims) zilindwe kwa nguvu zote. Hii ni kuhakikisha kuwa wasichana na wanawake waliofanyiwa ukatili huo hawaathiriki zaidi kisaikolojia kwa majina yao kuanikwa magazetini.


Sakata hili limechukua sura mpya ya kisiasa, huku Rais wa Marekani, Donald Trump, akiingia katika mjadala huo. Wakati wa kampeni zake, Trump alitumia kifo cha Epstein kama fimbo ya kuwapigia wapinzani wake, akidai kuwa kuna "mkono wa giza" (Deep State) uliohusika na kifo hicho. Hata hivyo, wakosoaji wanahoji ukimya wake au kigugumizi kinachoonekana sasa katika kutoa taarifa hizo, wakihisi huenda naye anahofia yatakayoibuka, ikizingatiwa kuwa alikuwa na ukaribu na Epstein miaka ya nyuma.


Wadadisi wa mambo wanasema kufunguliwa kwa mafaili haya kunaweza kuwa na athari kubwa kuliko inavyodhaniwa. Je, orodha hiyo itakuwa na majina ya Marais wa zamani, Wafalme, na Matajiri wakubwa kama inavyodaiwa kwenye nadharia za njama? Macho na masikio ya dunia nzima sasa yanaelekezwa New York, kusubiri tarehe 19 Desemba, siku ambayo inaweza kuwa ya kiama kwa heshima za vigogo wengi duniani.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.