Idara ya Ufanisi Serikalini ya Marekani (DOGE), inayoongozwa na bilionea na Mkurugenzi Mtendaji wa Tesla na xAI, Elon Musk, inakabiliwa na tuhuma nzito za kujaribu kushinikiza mashirika mengine ya serikali ya shirikisho kutumia mfumo wa Akili Mnemba (AI) wa kuzalisha maudhui (generative AI) unaoitwa 'Grok', ambao umetengenezwa na kampuni ya Musk, xAI. Hatua hii imezua mjadala mkubwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa mgongano wa kimaslahi, ukiukwaji wa faragha za kidijitali, na matumizi mabaya ya data nyeti.
Shirika la habari la Reuters, likinukuu vyanzo vingi vya habari Ijumaa iliyopita, tarehe 23 Mei 2025 (saa za Marekani), liliripoti kuwa Idara ya Ufanisi Serikalini (DOGE) imekuwa ikiyashinikiza mashirika kama Idara ya Usalama wa Taifa (DHS) kutumia Grok katika shughuli zao. Inadaiwa kuwa DOGE yenyewe inatumia toleo maalum la Grok kwa ajili ya kazi kama vile uchambuzi wa data, upembuzi, na uandishi wa ripoti. Shinikizo hili kwa DHS, ambayo inahusika na masuala kama usalama wa mipaka na usalama wa mtandao, linakuja hata kabla ya idara hiyo kuidhinisha rasmi matumizi ya Grok.
Vitendo hivi vinatajwa kuwa vinaweza kuipa xAI, kampuni ya Musk, faida isiyo ya haki katika sekta ya umma dhidi ya washindani wake kama OpenAI na Anthropic. Pia, imebainika kuwa iwapo wafanyakazi wa serikali ya shirikisho watapewa rasmi idhini ya kutumia Grok, watalazimika kulipia gharama za huduma hiyo.
Wasiwasi mkubwa zaidi umeibuka kuhusu usalama na faragha ya data wakati wa matumizi ya Grok. Tofauti na washindani wake, kampuni ya xAI ya Elon Musk imeweka wazi kwenye tovuti yake kuwa inaweza kufuatilia watumiaji wa Grok kwa madhumuni maalum ya kibiashara. Hii inazua hofu kuwa data nyeti za serikali na taarifa binafsi za Wamarekani zinaweza kuhamishiwa kwa xAI, ambayo ni kampuni ya kibinafsi. Aidha, haijulikani wazi ni nani hasa anayeweza kupata toleo hili maalum la Grok linalotumiwa na DOGE.
Zaidi ya hayo, kuna madai mazito zaidi kuwa idara ya Musk, DOGE, inatumia Akili Mnemba kwa ajili ya kufanya udhibiti na uchunguzi wa mawasiliano ndani ya serikali ya shirikisho. Vyanzo vya Reuters vinadai kuwa katika miezi ya hivi karibuni, maafisa wa DOGE wamejaribu kupata barua pepe za wafanyakazi wa DHS, wakitumia AI kufunza mfumo huo kutambua mawasiliano yanayodhaniwa kuonyesha ukosefu wa uaminifu kwa ajenda za kisiasa za Rais Trump. Kitendo hiki kinaweza kuwa ukiukaji wa sheria za utumishi wa umma. Hata hivyo, haijathibitishwa iwapo Grok ilitumika moja kwa moja katika shughuli hii mahususi.
Elon Musk, Ikulu ya White House, na kampuni ya xAI hawakujibu maombi ya Reuters ya kutoa maoni yao kuhusu tuhuma hizi. Msemaji wa Idara ya Usalama wa Taifa (DHS) alikanusha madai hayo kwa Reuters, akisema, "Hatujawahi kuwalazimisha wafanyakazi kutumia zana au bidhaa maalum," lakini hakujibu maswali zaidi. Kashfa hii inaibua maswali muhimu kuhusu mipaka ya matumizi ya AI serikalini na uadilifu wa viongozi wenye maslahi katika sekta binafsi.