Musk Arejea 'Ikulu' ya Trump kwa Kishindo, Bilioni 800 Zafanya Kazi

international | Wed Nov 19 2025


Musk Arejea 'Ikulu' ya Trump kwa Kishindo, Bilioni 800 Zafanya Kazi

Kuna msemo wa wahenga usemao, "Hasira za mkizi furaha ya mvuvi," lakini katika siasa za Marekani, hasira za mabilionea mara nyingi huishia kwenye meza ya mazungumzo, hasa pale maslahi na pesa ndefu vinapohusika. Miezi sita tu baada ya kufunga virago na kuondoka Washington D.C. kwa hasira, tajiri namba moja duniani, Elon Musk, anarejea katika viunga vya madaraka kwa kishindo, akiashiria kumalizika kwa 'bifu' kali kati yake na Rais Donald Trump.


Sherehe ya Ushindi na Kurudi Kundini


Kurejea huku si kwa kinyonge. Wiki hii, macho na masikio ya wachambuzi wa siasa yameelekezwa Washington na Texas. Huko Austin, Texas, timu nzima ya kile kinachoitwa "Wizara ya Ufanisi wa Serikali" (DOGE)—kitengo maalum kilichoundwa na Musk kusafisha uoza serikalini—inakutana kwa siku mbili kwenye hoteli ya kifahari kusherehekea kile wanachokiita mafanikio ya ushirikiano kati ya Musk na Trump.


Musk mwenyewe anatarajiwa kutua Washington usiku wa leo kwa mara ya kwanza tangu mwezi Mei, kuhudhuria chakula cha jioni cha hadhi ya juu (State Dinner) kilichoandaliwa na Rais Trump kwa ajili ya Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman (MBS). Mwaliko huu ni ishara tosha kuwa "yameisha na yamepita."


Chanzo cha Mtafaruku na Suluhu ya Pesa


Uhusiano wa vigogo hawa wawili ulivunjika miezi michache iliyopita katika hali ya kutatanisha. Musk aliondoka Washington akiwa amevimba, huku akitishia kuanzisha chama chake cha tatu cha siasa na hata kufukua makaburi ya kashfa za zamani zinazomhusu Trump na marehemu Jeffrey Epstein.


Hata hivyo, siasa ni mchezo wa namba na maslahi. Duru za ndani zinaeleza kuwa 'vita' hii imekwisha baada ya Trump kukubali kuwarudisha kazini washirika wa karibu wa Musk katika nafasi nyeti serikalini. Mfano mmoja wapo ni kuteuliwa tena kwa Isaacman kuongoza Shirika la Anga la Marekani (NASA), hatua iliyomfurahisha sana Musk ambaye anamiliki kampuni ya anga ya SpaceX.


Zaidi ya hayo, pesa imeongea. Ripoti zinaonyesha kuwa Musk alimwaga kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 300 (sawa na takriban Shilingi za Kitanzania Bilioni 780) ili kumsaidia Trump kushinda uchaguzi uliopita. Kwa kiasi hicho cha fedha, ni vigumu kwa wanasiasa kuweka kinyongo kwa muda mrefu. Inasemekana Musk amejiandaa kutoa kitita kingine kikubwa kwa ajili ya uchaguzi wa katikati ya muhula mwakani.


Biashara na Siasa: Mkono wa xAI Serikalini


Upatanisho huu hauji bure. Kampuni ya Akili Mnemba ya Musk, xAI, imetangaza kupata dili nono la serikali ambapo mashirika ya umma yatatumia teknolojia yake ya 'chatbot' kwa gharama nafuu. Hii ni 'win-win situation' (faida kwa pande zote); Trump anapata ufanisi na Musk anapata biashara na ushawishi.


Uhusiano ulianza kurudi vizuri mwezi Septemba, pale Musk alipohudhuria hafla ya kumbukumbu ya mwanaharakati Charlie Kirk na kuonekana akiteta na Trump kwa dakika kadhaa.


Mustakabali wa 2028: Urafiki na JD Vance


Wakati Musk akiwa na uhusiano wa "kupanda na kushuka" na baadhi ya maafisa wa Trump (kama alivyombwatukia Waziri wa Uchukuzi Sean Duffy kuwa anataka kuiua NASA), ameanzisha urafiki wa dhati na Makamu wa Rais, JD Vance.


Musk amekuwa akimwagia sifa Vance kwenye mtandao wake wa X, akisema ana "ladha nzuri ya mambo," hasa baada ya Vance kusifu teknolojia ya xAI. Wachambuzi wanaona hii kama hesabu za mbali; Vance anatajwa kuwa mgombea urais ajaye wa Republican mwaka 2028, na uungwaji mkono wa Musk—na pochi yake nzito—utakuwa turufu muhimu sana.


Kwa sasa, inaonekana Musk ameamua kuweka pembeni ndoto zake za kuanzisha chama kipya na badala yake kutumia nguvu na fedha zake kuendesha serikali akiwa nyuma ya pazia, huku akihakikisha maslahi ya biashara zake za anga na teknolojia yanalindwa kikamilifu.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.