Serikali ya Japan imeanza mchakato wa kujadili mabadiliko makubwa ya kisera yatakayoathiri moja kwa moja mamilioni ya watalii wanaotembelea nchi hiyo, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na kile kinachojulikana kama 'overtourism'—hali ya kuzidiwa na idadi kubwa ya watalii kupita kiasi.
Nchi hiyo ya Asia Mashariki imeshuhudia mlimbikizo wa wageni, hasa kutokana na kudorora kwa thamani ya sarafu yake (Yen) na hamu kubwa ya watu kusafiri duniani kote kufuatia kumalizika kwa vizuizi vya janga la UVIKO-19. Inakadiriwa kuwa idadi ya watalii wanaoingia Japan mwaka huu inaweza kufikia milioni 40. Hata hivyo, mfuriko huu umeleta changamoto kubwa, ikiwemo utupaji ovyo wa takataka, kelele zilizopitiliza, na watalii kuingia katika maeneo ya watu binafsi bila ruhusa, hasa katika miji maarufu kama Kyoto na Tokyo.
Ili kukusanya mapato yatakayotumika kupambana na kero hizi, pendekezo moja kubwa linalojadiliwa ni kuongeza "kodi ya kuondoka" (Departure Tax). Hivi sasa, kila msafiri—awe raia wa Japan au mgeni—analipa JPY 1,000 (takriban TZS 17,000) anapoondoka nchini humo. Mpango mpya unapendekeza kodi hii iongezwe kwa kiwango kikubwa, angalau mara tatu, na kufikia JPY 3,000 (takriban TZS 51,000) au hata zaidi.
Mapato yatakayotokana na ongezeko hili yataelekezwa moja kwa moja kwenye kuboresha miundombinu ya utalii, kuanzisha mifumo ya kudhibiti misongamano, na kuimarisha kampeni za kutoa elimu kwa watalii kuhusu kufuata sheria na kuheshimu utamaduni wa wenyeji.
Kwa kutambua kuwa kodi hii itaathiri pia raia wake, serikali inatafakari njia za kuwafidia Wajapani. Moja ya mapendekezo ni kupunguza ada ya kutoa pasipoti mpya ya miaka 10, ambayo kwa sasa ni JPY 15,900 (kama TZS 270,300). Kupunguzwa huku kunaweza kufikia JPY 10,000 (kama TZS 170,000) ili kupunguza makali kwa raia wake wanaosafiri kimataifa.
Mabadiliko mengine makubwa yanayolengwa ni kwenye mfumo wa ununuzi wa bidhaa bila kodi (Duty-Free au Tax-Free). Hivi sasa, watalii wanaweza kununua bidhaa katika maduka takriban 63,000 nchi nzima na kurudishiwa mara moja Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya 10% hapo hapo dukani. Hata hivyo, mfumo huu umebainika kutumiwa vibaya na baadhi ya watu wasio waaminifu.
Ripoti zinaonyesha kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukwepaji kodi, ambapo baadhi ya watalii hununua bidhaa nyingi (kama vile vipodozi na saa za bei ghali) bila kodi, na kisha kuziuza ndani ya Japan kabla ya kuondoka, wakijipatia faida kinyume cha sheria. Takwimu za Wizara ya Fedha ya Japan zilionyesha kuwa katika kipindi cha miaka miwili, watu 690 walinunua bidhaa zisizo na kodi zenye thamani ya zaidi ya JPY Milioni 100 (zaidi ya TZS Bilioni 1.7) kila mmoja, na kufanya jumla ya manunuzi yao kufikia JPY Bilioni 233.2 (takriban TZS Trilioni 4), huku kukiwa na shaka kubwa kama kweli bidhaa zote hizo ziliondoka nchini.
Ili kuziba mwanya huu, serikali inapendekeza kubadili mfumo kabisa. Kuanzia mwaka ujao (2025), watalii watalazimika kulipia bei kamili ya bidhaa (pamoja na kodi ya 10%). Watakapofika uwanja wa ndege kwa ajili ya safari ya kurudi, watahitajika kuonyesha bidhaa walizonunua kwa maafisa wa forodha, na ndipo watarudishiwa kodi yao baada ya uhakiki.
Vilevile, Japan inapanga kuongeza kwa kiasi kikubwa ada za maombi ya visa kwa wageni, hatua ambayo haijafanyika tangu 1978, ili viwango vyake viendane na vile vya nchi za Ulaya na Marekani.
Wakati hatua hizi zinalenga kulinda mazingira na utulivu wa nchi, baadhi ya wadau kwenye sekta ya utalii wana wasiwasi kuwa mabadiliko haya, hasa usumbufu wa utaratibu mpya wa kurejesha kodi uwanja wa ndege, yanaweza kuwafanya baadhi ya watalii wasichague tena Japan kama eneo la kutembelea.