Dunia inaenda kasi sana, na China imeamua kutoa "kioo" cha kutazamia jinsi nyakati zinavyoweza kubadilika ghafla. Baada ya miongo kadhaa ya kusifika kwa sera zake kali za kudhibiti idadi ya watu, taifa hilo la Asia Mashariki sasa limegeuza kibao na kuja na mbinu mpya inayowashangaza wengi: kuviwekea kodi vifaa vya kujikinga na mimba ili kuhamasisha wananchi kuzaana.
Kwa zaidi ya miaka 30, China imekuwa 'peponi' ya vifaa vya uzazi wa mpango, ambapo kondomu na vidonge vya kuzuia mimba vilikuwa havitozwi kodi (tax-free) kama sehemu ya mkakati wa taifa hilo kupunguza mlipuko wa watu. Hata hivyo, kuanzia Januari Mosi mwakani, "vya bure vimeisha". Bunge la China (National People's Congress) limepitisha sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambapo sasa kondomu na vidonge vya uzazi vitatozwa kodi ya asilimia 13.
Kutoka 'Mtoto Mmoja' hadi 'Zaeni Mjaze Nchi'
Hatua hii imekuja kama 'mshtuko wa umeme' kwa wachambuzi wa mambo, ikizingatiwa kuwa China ilijijengea umaarufu mwaka 1993 kwa sera yake ya "Mtoto Mmoja" (One Child Policy). Lakini sasa, serikali hiyo inaonekana kutumia mbinu ya 'fimbo na karoti'. Wakati ikiongeza gharama kwenye kondomu, kwa upande mwingine imefuta kodi kwenye huduma za malezi ya watoto (daycare), shule za awali, huduma za ndoa, na utunzaji wa wazee.
Lengo liko wazi: Serikali inataka kupunguza mzigo kwa wale wanaoamua kuoa na kuzaa, huku ikiongeza gharama kwa wale wanaotaka "kula ujana" bila kuzaa.
Kilio cha Uchumi na Gharama za Maisha
Sababu kuu ya mabadiliko haya ni hofu kubwa ya kiuchumi. China inakabiliwa na anguko la kutisha la idadi ya watoto wanaozaliwa. Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka jana, idadi ya watoto waliozaliwa ilishuka hadi kufikia milioni 9.54, ikiwa ni pungufu ya nusu ya watoto milioni 18.8 waliozaliwa miaka kumi iliyopita. Hii ni hatari kwa taifa ambalo nguvukazi yake inazeeka kwa kasi.
Hata hivyo, vijana wa China wanalia na "vyuma kukaza". Taasisi ya Yuwa Population Research inakadiria kuwa gharama ya kulea mtoto mmoja nchini humo hadi kufikia utu uzima ni takribani Yuan 538,000 (sawa na zaidi ya Shilingi za Kitanzania Milioni 193). Kwa kijana anayepambana na ukosefu wa ajira na gharama za maisha, fedha hiyo ni "mlima Kilimanjaro" kuupanda.
Hofu ya Magonjwa na Ukimwi
Wakati serikali ikitazama namba za uchumi, wataalam wa afya wanatazama namba za maafa. Uamuzi wa kupandisha bei ya kondomu unatajwa kuwa na hatari ya kuchochea "bomu" lingine la afya.
Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha China kimeonya kuwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) yanaongezeka kwa kasi. Takwimu zinaonyesha kuwa maambukizi yamepanda kutoka wastani wa watu 0.37 kwa kila watu 100,000 mwaka 2002, hadi kufikia watu 8.41 mwaka 2021.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini humo wamecharuka, wakidai kuwa ongezeko la bei ya kondomu linaweza kusababisha mimba zisizotarajiwa kwa wingi na mbaya zaidi, kuongeza kasi ya maambukizi ya magonjwa ya zinaa kwa vijana wasiomudu gharama mpya. Hii inazua mjadala mzito: Je, ni bora kuwa na taifa lenye watu wengi wagonjwa au watu wachache wenye afya?
Wakati China ikijaribu kila mbinu—kuanzia kutoa pesa taslimu kwa wazazi, kuongeza likizo ya uzazi, na sasa kuweka kodi kwenye kondomu—bado haijulikani kama vijana wa kisasa watakubali kubadili mtindo wao wa maisha kwa ajili ya sera za serikali.