Serikali ya mrengo wa kulia nchini Italia, inayoongozwa na Waziri Mkuu Giorgia Meloni, inajiandaa kuwasilisha muswada wa sheria utakaopiga marufuku uvaaji wa mavazi ya Kiislamu yanayofunika mwili na uso mzima, kama vile burqa na niqab, katika maeneo yote ya umma nchini humo. Hatua hii inaifanya Italia kuwa nchi nyingine kubwa barani Ulaya kutaka kufuata mkondo ulioanzishwa na Ufaransa zaidi ya muongo mmoja uliopita.
Kwa mujibu wa chama tawala cha Brothers of Italy (FdI), sheria hiyo inapendekezwa kama njia ya kupambana na kile walichokiita "utengano wa Kiislamu" na kulinda kanuni za kitaifa. Mtu yeyote atakayepatikana akikiuka sheria hiyo endapo itapitishwa, atakabiliwa na faini kali inayoweza kufikia Euro 3,000 (takriban Shilingi za Kitanzania milioni 8.4).
Mbunge Andrea Delmastro, mmoja wa watetezi wakuu wa muswada huo, alieleza kuwa walipata msukumo kutoka kwa sheria ya Ufaransa ya mwaka 2011. "Uhuru wa dini ni mtakatifu, lakini ni lazima utekelezwe kwa kuheshimu kikamilifu katiba yetu na misingi ya taifa la Italia," alisema Delmastro. Aliongeza kuwa sheria hiyo inatokana na imani kwamba "hakuna ufadhili wa kigeni unaopaswa kudhoofisha mamlaka au ustaarabu wetu."
Mavazi yanayolengwa na sheria hii ni pamoja na burqa, vazi linalofunika mwili mzima kuanzia kichwani hadi miguuni huku macho yakiwa na kifuniko cha wavu, na niqab, ambayo ni shela inayofunika uso isipokuwa eneo la macho.
Sara Kelani, mkuu wa idara ya uhamiaji katika chama cha FdI, alifafanua kuwa muswada huo pia unalenga kudhibiti vyanzo vya ufadhili wa misikiti na kuimarisha sheria dhidi ya ndoa za kulazimishwa.
Ufaransa ilikuwa nchi ya kwanza Ulaya kupiga marufuku mavazi hayo mwaka 2011 chini ya utawala wa Rais Nicolas Sarkozy. Marufuku hiyo inajumuisha maeneo yote ya umma kama vile ofisi za serikali, hospitali, shule, maduka makubwa, na vyombo vya usafiri. Licha ya kuzua mjadala mkubwa, sheria hiyo ilithibitishwa na mahakama za Ufaransa na baadaye Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya (ECHR), ambayo iliamua kuwa haikukiuka haki ya uhuru wa dini. Nchi nyingine za Ulaya kama Ubelgiji, Denmark, na Uswizi zimefuata na kuanzisha marufuku kamili au kiasi.