Wanandoa waliokuwa waajiri wa msichana wa miaka 13 nchini Pakistan wamekamatwa kwa tuhuma za kumuua baada ya kumshutumu kwa kuiba chokoleti.
Kwa mujibu wa ripoti ya BBC tarehe 18, msichana huyo, aliyefahamika kwa jina Iqra, alifariki tarehe 5 mwezi huu akiwa hospitalini kutokana na majeraha mengi mwilini. Uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa aliteswa kabla ya kifo chake.
Kifo cha Iqra kimeibua ghadhabu kubwa kote Pakistan, huku maelfu ya watu wakitumia alama ya reli #JusticeForIqra kwenye mitandao ya kijamii kulaani unyanyasaji wa wafanyakazi wa nyumbani na ajira za watoto.
Kwa mujibu wa sheria za jimbo la Punjab, ni marufuku kuwaajiri watoto wa chini ya miaka 15 kama wafanyakazi wa nyumbani. Baba wa Iqra, Sana Ullah, alisema: "Kifo cha binti yangu kimenivunja moyo kabisa. Polisi walinipigia simu tarehe 5 na kunijulisha kuhusu hali yake. Nilipofika hospitalini, Iqra alikuwa amelala kitandani bila fahamu, na dakika chache baadaye, akafariki."
Iqra alianza kufanya kazi akiwa na umri wa miaka 8 kutokana na madeni ya baba yake, ambaye ni mkulima mwenye kipato cha chini. Miaka miwili iliyopita, alipelekwa kufanya kazi katika nyumba ya wanandoa wenye watoto wanane, ambapo alikuwa akilipwa mshahara wa dola 23 tu kwa mwezi (takriban shilingi 30,000 za Kenya).
Polisi wanasema kuwa ushahidi unaonyesha kuwa Iqra alinyanyaswa mara kwa mara. BBC imepata picha na video zinazoonyesha majeraha makubwa mwilini mwake, ikiwa ni pamoja na kuvunjika kwa mifupa ya mikono na miguu pamoja na majeraha mabaya kichwani.
Mamlaka zinafanya uchunguzi zaidi, huku ripoti ya kitabibu ikisubiriwa ili kuthibitisha chanzo halisi cha kifo chake.
Tukio hili limeibua hisia kali kwa wanaharakati wa haki za binadamu. Sher Bano, mtetezi wa haki za binadamu nchini Pakistan, alisema: "Moyo wangu unavuja damu. Ni wangapi zaidi wanaopaswa kuteswa na kuuawa kwa sababu zisizo na maana? Je, maskini wataendelea kupoteza watoto wao kwa njia hii hadi lini?"
Baadhi ya raia wa Pakistan kwenye mitandao ya kijamii wamelaani kifo cha Iqra, wakisema kuwa sio tu uhalifu wa mtu binafsi bali ni ishara ya mfumo kandamizi unaowaruhusu matajiri kuwadharau maskini.
Polisi wamewakamata waajiri wa Iqra, Rashid Shafiq na mkewe Sana, pamoja na mwalimu wa Qur’an wa familia hiyo, ambaye ndiye aliyempeleka hospitalini kabla ya kudai kuwa wazazi wake hawapo na kisha kutoweka.
Baba yake Iqra amesema anataka wahusika wawajibishwe: "Sitapumzika mpaka haki ya binti yangu ipatikane."
Hata hivyo, wanaharakati wameeleza wasiwasi wao kuwa kesi hii huenda ikamalizwa nje ya mahakama kwa makubaliano ya kifedha, jambo ambalo ni la kawaida nchini Pakistan. Sheria ya nchi hiyo inaruhusu familia za waathiriwa kusamehe watuhumiwa, mara nyingi baada ya kulipwa fidia ya kifedha, na hili limefanya kesi nyingi za mauaji kutoishia kwenye hukumu kali.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), takriban watoto milioni 3.3 wanateseka kutokana na ajira za utotoni nchini Pakistan. Aidha, ripoti ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) inakadiria kuwa kati ya wafanyakazi wa nyumbani milioni 8.5 nchini humo, wengi wao ni wanawake na wasichana wadogo, wengi wakiwa katika mazingira ya unyonyaji na ukatili.