Taifa la Uzbekistan limekumbwa na mshtuko mkubwa kufuatia taarifa za mwanamke mmoja kukamatwa kwa tuhuma za kumchoma kisu na kumuua binti yake wa miaka saba, mwanamke huyo akiwa ni yuleyule aliyeshtua ulimwengu miaka mitatu iliyopita kwa kumtupa mtoto huyo kwenye zizi la dubu katika bustani ya wanyama.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa, Zilola Tulyaganova (34) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua binti yake kwa kutumia kisu cha jikoni. Inaripotiwa kuwa mtoto huyo alipata jeraha baya la kisu shingoni, na mwili wake uligunduliwa na babu yake aliporejea nyumbani, ambaye ndiye aliyetoa taarifa polisi.
Tukio hili la kutisha limefufua kumbukumbu za tukio la mwaka 2022, ambapo Tulyaganova alinaswa na kamera za usalama (CCTV) akimnyanyua binti yake, aliyekuwa na umri wa miaka mitatu wakati huo, na kumrusha kutoka umbali wa takriban mita 4.8 kwenda chini kwenye zizi la dubu mkubwa.
Katika tukio hilo la awali, mtoto alinusurika kimiujiza. Dubu huyo hakumshambulia; alimsogelea, akamnusa, na kisha akaondoka zake. Wafanyakazi wa bustani ya wanyama walichukua hatua za haraka kumshawishi dubu aingie ndani ili waweze kumwokoa mtoto. Binti huyo alipata majeraha kichwani lakini alipona kabisa baada ya kupatiwa matibabu kwa wiki tatu.
Wakati huo, Tulyaganova alichunguzwa kwa jaribio la mauaji. Hata hivyo, hakushtakiwa baada ya uchunguzi wa afya ya akili kuhitimisha kuwa alikuwa ‘salama’ na mwenye uwezo wa kuendelea kuwalea watoto wake. Uamuzi huo sasa umezua maswali na mjadala mkali nchini humo.
Miaka mitatu tu baada ya kuonekana hana hatia, mama huyo sasa anakabiliwa na tuhuma nzito za mauaji, kitendo ambacho kimeacha jamii nzima katika hali ya sintofahamu na majonzi makuu.